Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​PROF. MBARAWA ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA MRADI WA SGR MWANZA - ISAKA


news title here
25
November
2023

Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR kipande cha tano Mwanza – Isaka alipofanya ziara kukagu mradi wa SGR kuanzia Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga, Novemba 24, 2024.

Mradi wa SGR Mwanza – Isaka una urefu wa kilomita 341, kilomita 249 za njia kuu na kilomita 92 za njia za kupishana na unajengwa kwa Dola za kimarekani takribani bilioni 1.321 ambazo ni sawa na trilioni 3.45 chini ya mkandarasi kampuni ya CCECC na CRCC kutoka nchini China.

“Nimetembelea mradi na nimeridhika sana kwasababu mandarasi huyu amejipanga, ukienda kwenye miradi mingi utakuta wakandarasi wamelala kipindi hiki cha mvua lakini mkandarasi huyu anafanya kazi na ndivyo wakandarasi wanatakiwa kufanya kazi, unapanga kazi kulingana na misimu, kipindi cha jua kali unajenga tuta, kipindi cha mvua unafanya kazi kama hizi za kuweka mataruma, reli na nguzo za umeme” alisema Prof. Mbarawa

Prof. Mbarawa amesema kuwa Mhe. Rais anafanya jitihada kuhakikisha miradi ya kimkakati inakwenda kwa kasi na Serikali itahakikisha inafanya kila kinachowekana kulipa wakandarasi kwa wakati

Mhe. Christina Mdeme, Mkuu wa mkoa wa Shinyanga amesema kuwa mkoa wa Shinyanga ni wanufaika wakubwa wa mradi wa SGR ambao unapita katika wilaya za Shinyanga, Kahama na Kishapu hivyo wamejipanga kuandaa mazingira ya kuzitumia fursa za mradi pindi utakapokamilika. Pia Mhe. Mdeme ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kulinda mali na miundombinu ya reli ili kufikia adhma ya Mhe. Rais ya kuboresha huduma ya usafirishaji.

Kamimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Bwana Focus Sahani amesema kuwa “Tupo kwaajili ya ugeni wa waziri wetu wa uchukuzi, kama mlivyoelezwa mradi umefikia asilimia 44.23 sisi kama TRC tumekuja kupata maelekezo lakini kama mlivyoona mradi unaendelea vizuri na kufikia mwaka 2024 tunatarajia kukamilisha mradi”

Mradi wa SGR Mwanza – Isaka unaendelea, kazi kubwa ya ujenzi wa tuta imekamilishwa kwa zaidi ya asilimia 80, ujenzi wa majengo ya stesheni na madaraja, uwekaji reli na mataruma unaendelea ambapo utandikaji wa reli umefikia kilomita 24. Kukamilika kwa mradi wa SGR Mwanza – Isaka kunatarajiwa kuleta fursa za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa ya kanda ya Ziwa pamoja na kuifungua nchi kupitia biashra na nchi jirani za Uganda, Kenya, Burundi na Rwanda kupitia usafiri na usafirishaji wa njia ya reli.