PROF. MBARAWA AIPONGEZA TRC KWA USIMAMIZI MZURI WA MRADI WA SGR
March
2022
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa amelipongeza Shirika la Reli Tanzania – TRC kwa usimamizi mzuri wa mradi wa reli ya kisasa – SGR alipofanya ziara katika mradi wa SGR kipande cha Dar es Salaam – Morogoro kuanzia Dar es Salaam hadi Kwala mkoani Pwani Machi 3, 2022.
Mhe. Prof. Mbarawa amefanya ziara hiyo katika kuadhimisha mafanikio ya sekta ya reli katika kipindi cha mwaka mmoja cha Uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa SGR kwa kuona kuwa upo mbioni kukamilika ili majaribio yaanze kufanyika.
Mhe. Prof. Mbarawa alisema kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kwenye sekta ya Uchukuzi katika kipindi cha mwaka mmoja kwa kusaini mikataba pamoja na serikali kutenga fedha nyingi katika kufanikisha ujenzi wa reli.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais amefanya kazi kubwa kwenye hii sekta ya Ujenzi na Uchukuzi” alisema Mhe. Prof. Mbarawa.
Aidha Mhe. Prof. Mbarawa amelitaka Shirika la Reli kuhakikisha mradi wa SGR Dar es Salaam – Morogoro unakamilika na kuongeza kuwa matarajio ni kuanza majaribio mwezi Aprili na baadaye huduma kuanza rasmi
“Tunatarajia mwisho wa mwezi wa nne treni ya umme ianze majaribio, ili kujiridhisha kwamba njia pamoja na mitambo yote ipo sawa ndio itaanza kubeba abiria“ alisema Mhe. Prof. Mbarawa.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ameeleza kuwa kipande kilichobaki cha ujenzi ni kipande cha kuweka njia za juu katika maeneo ya Vingunguti, Airport pamoja na Banana.
“Ni asilimia ndogo ya ujenzi ambayo imebaki, mwezi wa kumi mwaka jana tumeanza majaribio ya umeme, nyaya za mawasiliano, makalavati, umeme wa kwenye majengo” alisema Ndugu Kadogosa.
Hata hivyo Ndugu Kadogosa ameeleza kuwa mara kwanza kulikua na majaribio ya kichwa cha mkandarasi kinachotumia mafuta (diesel) ambapo sasa hivi majaribio yatakayofanyika ni ya kichwa cha umeme cha mkandarasi ambacho kimeshawasili nchini hivi karibuni.
Ziara hii kukagua mradi wa SGR inakuwa ya kwanza kwa Mhe. Prof. Mbarawa tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ambapo pamoja na mambo mengine Mhe. Waziri ameridhishwa na maendeleo ya mradi huo lakini pia ametoa maagizo kwa uongozi wa Shirika kuendelea kusimamia vyema mradi ili uweze kukamilika.