Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​PROF. KONDORO ATAMBULISHA WAJUMBE WAPYA BODI YA WAKURUGENZI TRC


news title here
17
February
2023

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Shirika la Reli Tanzania – TRC Prof. John Wajanga Kondoro ametambulisha wajumbe wapya wa bodi ya wakurugenzi TRC na kuwaaga wajumbe waliomaliza muda wao katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya makao makuu TRC jijini Dar es Salaam, Februari 2023.

Wajumbe wapya wa Bodi ya Wakurugenzi TRC waliotambulishwa ni Bw. Benjamini Adam Mbimbi, Bw. Kondo Abdalah Kibugula, Bw. Joseph Elias Salema, Bw. Juma Samhando Kijavara na Bw. Peter Mayunga Noni. Wajumbe waliomaliza muda wao ni Bw. Wolfgang Ephraim Salia, Bi. Consolata Chrisostom Ngimbwa, Bw. Karim Godfrey Mattaka, Bw. Rogatus Hussein Mativila na Bw. Mahamud Mashaka Mabuyu.

Mwenyekiti wa Bodi Prof. Kondoro kwa niaba ya uongozi wa TRC amewashukuru wajumbe waliomaliza muda wao kwa mchango waliotoa kipindi chote walichokuwa katika nafasi za ujumbe na kuliwezesha Shirika kupiga hatua na kuongeza ufanisi katika utendaji wa Shirika.

“Lengo la kukutana hapa ni kutambuana na kutambua mchango wa wajumbe ambao wamelitumikia Shirika la Reli, waliingia katika kipindi ambacho tulikuwa kwenye sekeseke kuhusu maendeleo ya mradi wa SGR na mpaka tulipofika hapa, kwahiyo ni vyema kutambua mchango wao lakini pia kuwashukuru na kuwakaribisha wajumbe wapya” alisema Prof. Kondoro

Wajumbe wanaoendelea na nafasi zao ni pamoja na Bw. Jabir Bakari na Bi Lilian Ngilangwa. Baadhi ya wajumbe waliomaliza muda wao walipata fursa ya kutoa neon kwa menejimenti ya Shirika na kupongeza jitihada kubwa zilizofanywa kuhakikisha watumishi wanafanya kazi kwa weledi na kuleta tija katika utendaji wa Shirika.

“Nataka niwapongeze sana menejimenti hususani Mkurugenzi Mkuu, tunashukuru kwamba mradi unaendelea na vipande vyote vina wakandarasi, awali niliona menejimenti ni ndogo lakini nikupongeze Mwenyekiti kwa kuboresha muundo wa Shirika” alisema Bi. Consolata

Aidha, wajumbe wapya wamepata fursa ya kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma kwa lengo la kufahamu namna mradi wa SGR unavyotekelezwa na Shirika la Reli Tanzania.

“Lengo la ziara ni kwamba tumepata wajumbe wapya wa bodi, hivyo ni vizuri kuwapitisha wakajua mifumo na miundombinu watakayokuwa wanaisimamia ikiwemo hii SGR, hii ni sehemu ndogo tu lakini wakati mwingine watapata kutembelea maeneo mengine” alisema Prof. Kondoro.