Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI ATEMBELEA TRC


news title here
13
September
2023

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Mwakiposa Kihenzile atembelea Shirika la Reli Tanzania - TRC na kufanya kikao kifupi na menejimenti ya TRC katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya TRC jijini Dar es Salam Septemba 13, 2023.

Mhe. Kihenzile alisema kuwa lengo ni kujitambulisha na kujionea kazi zinazofanywa na Shirika la Reli Tanzania ili kupata uelewa utakaomsaidia katika kutekeleza majukumu yake ndani ya Wizara.

“Nimepata fursa ya kusikiliza historia ya TRC na maendeleo ya mradi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR, viongozi pamoja na wafanyakazi wa TRC wanastahili pongezi kwa usimamizi makini wa mradi wa SGR kwa vipande vyote vitano vya awamu ya kwanza kutoka Dar es salaam had Mwanza” alisema Mhe. Kihenzile.

Mhe. Kihenzile alieleza kuwa TRC inatakiwa kuongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo ili kuongeza pato la taifa, pia Shirika linatakiwa lihakikishe kunakuwa na thamani halisi ya bidhaa zinazonunuliwa pamoja na muda wa mikataba ya miradi mbalimbali uzingatiwe ili uendeshaji uanze kwa wakati.

“Mwenyezimungu ametujaalia nchi ambayo ina jografia nzuri, tuna bandari inayotegemewa na nchi nyingi zinazotuzunguka, suluhisho la kuwafikishia mizigo yao kwa haraka ni SGR" alisema Mhe. Kihenzile.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa TRC Bi. Amina Lumuli alieleza kuwa ujenzi wa mradi wa reli yenye kiwango cha kimataifa una vipande vitano, kipande cha kwanza kutoka Dar es salaam - Morogoro kina urefu wa kilometa 300 ujenzi wake umefikia asilimia 98.45 , kipande cha pili ni kutoka Morogoro - Makutopora kina urefu wa kilometa 422 ujenzi umefikia asilimia 94.99 , kipande cha tatu kutoka Makutopora - Tabora urefu wake ni kilometa 368 ujenzi umefikia 10.92 , kipande cha nne kutoka Tabora - Isaka chenye urefu wa kilometa 165 ujenzi umefika asilimia 4.63 na kipande cha tano kutoka Isaka - Mwanza chenye urefu wa kilometa 341 ujenzi wake umefikia asilimia 37.22.

Aidha, Bi. Amina alisema kuwa wakandarasi wanaendelea na kazi kwenye vipande vyote vitano ya ujenzi wa SGR awamu ya kwanza kutoka Dar es salaam hadi Mwanza na vilevile ujenzi huo wa SGR kwa awamu ya pili una vipande vinne, kipande cha kwanza kutoka Tabora - Kigoma chenye urefu wa kilometa 506 mkandarasi ameshaanza atua za awali za ujenzi, na vipande vilivyobaki tayari umeshafanyika usanifu wa awali na upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuanza ujenzi.

"Mradi wa SGR umetoa ajira zaidi ya laki moja za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa watanzania na kuwa chachu ya uchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kwa sababu vifaa vya ujenzi kama saruji na nondo vinavyotumika kwenye mradi vinatoka hapa nchini" alisema Bi Amina.

Mwakiposa ni Naibu Waziri mpya wa Uchukuzi aliyeteuliwa tarehe 30/08/2023 kufuatia mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri yaliyofanywa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.