Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA MRADI WA SGR


news title here
10
April
2021

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara aridhishwa na maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR Morogoro – Makutupora ambao ujenzi wake umefikia 57.5%, Aprili 10, 2021.
Mhe. Waitara ameyasema hayo alipokuwa katika ziara yake kukagua mradi wa SGR Kilosa mkoani Morogoro, ambapo ziara hiyo ya siku mbili inahusisha ukaguzi wa Mradi kwa kipande cha Morogoro – Makutupora na Dar es Salaam – Morogoro kwa lengo la kuona mwenendo wa mradi huo.
Mhe. Naibu Waziri ameeleza kuwa ameridhishwa na maendeleo ya mradi huo wa kimkakati kwakuwa kazi zinakwenda vizuri na watanzania wananufaika na mradi wakati huu wa ujenzi na hata mradi utakapokamilika.
“Leo nimefanya ziara kujiridhisha na kazi inayoendelea katika kipande hiki cha pili cha ujenzi wa reli hii ya kisasa kutoka Dodoma hadi Morogoro, nimeridhishwa kwamba kazi inakwenda vizuri na nimefurahi kwakuwa vijana wetu wazawa wapo kazini wanafanya kazi jambo ambalo litasaidia pindi wakandarasi watakapoondoka tutakuwa na wataalamu watakaosimamia mradi huu” alisema Mhe. Waitara.
Aidha, Mhe Waziri amewataka wafanyakazi wazawa wanaoshiriki katika mradi kuwa walinzi wa vifaa na malighafi zinazotumika katika mradi huo, kwakuwa uzalendo na uaminifu wao utaweza kuwanufaisha katika kupata fursa za ajira hapo baadae, pia itasaidia mradi huo kukamilika na hatimaye kuwanufaisha watanzania
“Watanzania mliopata fursa kufanya kazi katika mradi mna jukumu la kulinda vifaa na mitambo inayofanya kazi hapa, tunaamini kwamba ninyi ni waaminifu na serikali inaamini hivyo” aliongeza Mhe. Waitara
Halikadhalika, Mhe. Naibu Waziri alieleza kuwa “Mradi huu utakapokamilika kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, muonekano wa nchi yetu utabadilika sana, uchumi wetu utakua, tutaongeza watalii wa ndani na nje hivyo nawasihi watanzania waendelee kuwa na imani na Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia kuwa Miradi yote ya kimkakati itakamilika”
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa ameshukuru ujio wa Mhe. Naibu Waziri kwa kusema kuwa “Namshukuru sana Mhe. Waziri kwa kuona kinachoendelea na kuridhishwa na kazi, sambamba na hayo ametoa maelekezo ambayo ni lazima tuyafanye kwa utiifu na uzalendo”
Kadogosa alisisitiza kuwa mpaka sasa Mradi huo kwa kipande cha Morogoro – Makutupora umeshafikia 57.5%, ujenzi unaendelea kwa kasi na lengo ni kuunganisha Ihumwa na Pugu ifikapo mwezi Agosti 2021, Kadogosa ameahidi kuwa Shirika litaendelea kusimamia Mradi kwa nguvu zote, kwa uzalendo na kwa utii wa serikali na nchi.