NAIBU WAZIRI UCHUKUZI APONGEZA TRC KWA KASI YA UKARABATI WA MIUNDOMBINU YA RELI
February
2024
Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile ametembelea TRC kukagua reli ya kati kutoka Lukobe Morogoro hadi Gulwe Mkoani Dodoma akiambatana na wahandisi na maafisa kutoka TRC wanaosimamia ukarabati wa miundombinu ya reli katika maeneo hayo tarehe 3 Februari 2024.
Mhe. David Kihenzile amefanya ukaguzi wa miundombinu ya reli ya kati katika maeneo ya Lukobe, Munisagara, Mzaganza, Kidibo na Gulwe iliyoathirika kutokana na mvua kubwa kunyesha kuanzia tarehe 25 Januari 2024 na kusababisha Shirika la Reli Tanzania kusimamisha usafiri wa treni za abiria na usafirishaji wa mizigo kuelekea Kigoma, Mwanza na Mpanda kupitia Morogoro na Dodoma kutoka Dar es Salaam.
Naibu Waziri David Kihenzile ameipongeza timu ya TRC kwa kuendelea kufanya ukarabati wa miundombinu ili kurejesha mawasiliano ya njia ya reli.
Mhandisi kutoka TRC Bwana Oswin Matanda ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa kuendelea kutoa fedha za miradi hususani katika kipindi cha dharura.
"Wafanyakazi wa TRC kwa kushirikiana na uongozi wa TRC wamefanya jitihada nyingi usiku na mchana kurudisha mawasiliano ya reli kutoka tarehe 26 Januari 2024 hadi tarehe 02 Februari 2024" ameongeza Mhandisi Matanda.
Meneja Mradi Kipande cha Kilosa - Gulwe reli ya kati Mhandisi Faraja Yusto amesema timu ya ukarabati wa njia ya reli imefanya marekebisho makubwa ikiwemo uchepushaji wa njia kwa ajili ya kurudishia njia iliyokua imeathirika na athari ya mvua kubwa na zoezi hili limefanywa kwa siku 8 na ukarabati bado unaendelea ikiwemo uchepushaji na uimarishaji wa mto ili kuepusha reli isiathiriwe na maji.
"Kutoka tarehe 26 hadi tarehe 30 tulikua kipande cha Godegode na Gulwe ambapo mita 300 ziliharibiwa na mvua pia kuanzia tarehe 30 hadi leo tarehe 03 Februari 2024 tumefanikiwa kurudishia njia Mzaganza kwahiyo hadi leo tumefanikiwa kurudishia kipande cha kilomita moja na tunategemea Hadi kufikia tarehe 4 Februari 2024 hali ya njia itakua salama" amesisitiza Mhandisi Faraja.
TRC imeingia mkataba na CCECC kwaajili ya ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 175 Godegode na njia zake za kilomita 6.2 kuelekea Gulwe ili kusaidia kuondoa tatizo la kujaa kwa mchanga Godegode na hii itaweka suluhisho la kudumu katika kipande hicho na Serikali imetenga bilioni 33 ambapo hadi sasa mkandarasi ameshalipwa malipo ya awali.