Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MSEMAJI MKUU WA SERIKALI AELEZEA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA KIMKAKATI


news title here
27
August
2023

Msemaji Mkuu wa Serikali Ndugu Gerson Msigwa amekutana na waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika katika jengo la stesheni ya SGR lililopo jijini Dar es Salaam na kuzungumzia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ukiwemo mradi wa ujenzi wa reli yenye kiwango cha kimataifa – SGR Agosti 26, 2023.

Ndugu Msigwa alisema Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania – TRC inaendelea na utekelezaji wa mradi huo wa SGR kwa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza una takribani kilometa 1219 na awamu ya pili kutoka Tabora hadi kigoma ni kilometa 506.

Awamu ya kwanza na ya pili ya ujenzi wa SGR nchini zinaifanya Tanzania kuwa nchi inayojenga mtandao mrefu zaidi wa reli ya kisasa barani Afrika (zaidi ya KM 2100), huku ikiwa miongoni mwa nchi chache za Afrika zinazotumia nishati ya umeme na teknolojia ya kisasa zaidi ya uendeshaji wa reli duniani (ERTMS Level ii)” alisema Ndugu Msigwa.

Aidha, Ndugu Msigwa alisema kuwa awamu ya pili ya ujenzi wa SGR kipande cha kutoka Tabora – Kigoma mkandarasi anaendelea na kazi za awali za maandalizi ikiwemo ukusanyaji wa vifaa na ujenzi wa kambi za ujenzi hali kadhalika zoezi la utwaaji wa ardhi na ulipaji fidia kwaajili ya ujenzi wa kambi zote tatu za Urambo, Nguruka na Uvinza limekamilika.

Vilevile, Ndugu Msigwa alieleza kuwa kupitia mkataba wa ununuzi wa mabehewa 30 na vichwa 2 vya treni kutoka kampuni ya Leuckemeire ya nchini Ujerumani, tayari mabehewa 6 yamekweishaingia nchini, mabehewa 24 yaliyobaki na vichwa 2 vinaendelea kukarabatiwa nchini Ujerumani.

“Serikali imenunua aina tofauti za mabehewa 1,430 ya mizigo kwa ajili ya reli ya kisasa ambayo yanaendelea kutengenezwa na kampuni ya CRRC ya nchini China pia utengenezaji wa mabehewa 59 ya abiria kutoka kampuni ya SSRST ya Korea ya Kusini, unaendela vizuri ambapo mabehewa 14 kati ya hayo yameshaingia nchini na mabehewa 45 yanaendelea kutengenezwa nchini Korea” alieleza Ndugu Msigwa.

Hata hivyo Ndugu Msigwa alifafanua kuwa utengenezaji wa vichwa 17 vya treni ya umeme na seti 10 za treni za kisasa EMU kutoka kampuni ya Hyundai Rotem ya Korea ya Kusini, unaendelea vyema na serikali inaendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha kazi hiyo inakwenda kulingana na makubaliano.

“Kati ya vifaa vya uendeshaji tulivyokua tukitarajia kupokea mwishoni mwa mwezi wa saba ambavyo ni vichwa viwili vyenye kutumia nishati ya umeme kutoka nchini Ujerumani bado havijakamilika kutokana na changamoto ya baadhi ya vifaa ambavyo ni vipuli vilivyoagizwa nchini jirani kutopatikana kwa muda uliopangwa na kupelekea kuchelewesha utayari wa matumizi ya vichwa hivyo” alisema Ndugu Msigwa.

Thamani ya uwekezaji wa serikali katika mradi wa SGR mpaka sasa ni zaidi ya shilingi Trilioni 23 za Kitanzania ambapo awamu ya kwanza na ya pili ya ujenzi wa reli ya kisasa nchi, zitaifanya Tanzania kuwa nchi inayojenga mtandao mrefu zaidi wa reli ya kiwango cha kimataifa barani Afrika.