Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MRADI WA SGR WAPAMBA MOTO, TRENI YATEMBEA KUTOKA PUGU HADI KILOSA


news title here
13
September
2021

Kipande cha reli kutoka Pugu Dar es Salaam hadi Kilosa mkoani Morogoro chakamilika ambapo Waziri Mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amembelea kipande hiko cha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR chenye urefu wa kilometa 245 kutumia treni ya uhandisi ya mkandarasi kukagua mradi huo Septemba 12, 2021.

Waziri Mkuu amesema kuwa ziara hiyo imelenga kuikagua njia ya reli hiyo ya SGR kama ipo salama na imekamilika na pia kuhakikisha kuwa vituo vyote vilivyojengwa kwaajili ya abiria vimekamilika.

“Treni inayokuja itakuwa inasukumwa kwa umeme na nimejihakikishia uwepo wa nguzo kutoka huko na zimewekwa na nyaya“ alisema Mhe. Majaliwa.

Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa reli hiyo ya SGR itawekwa uzio kwa ajili ya usalama wa binadamu, mifugo na wanyama kwa kuwa treni hiyo itakuwa na kasi kubwa na haitaruhusiwa kwa mtu yeyote kukatiza ama kukaa karibu na eneo la reli ili kuepusha ajali zitakazojitokeza.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa vituo vyote vya stesheni vya awamu ya kwanza Dar es Salaam - Morogoro vimekamilika kuanzia cha Dar es Salaam, Pugu , Soga , Ruvu , Morogoro lakini pia kwa kipande cha pili Stesheni ya Mkata na Kilosa nazo zimekamilika

“Nimekagua jengo la abiria Dar es Salaam lijulikanalo kama Tanzanite, limekamilika kwa asilimia 100 “ alisema Mhe. Majaliwa.

Mhe. Majaliwa amesema kuwa wananchi wakae tayari kupokea behewa za treni za SGR ambazo zinatarijia kuwasili nchini mnamo mwezi Novemba na kuanza kufanyiwa majaribiao katika njia ya reli

Mhe. Majaliwa amewaeleza wananchi kutumia fursa za mradi huo kwa kuanzisha nyumba za wageni pamoja na biashara mbalimbali ili kuzidi kujipatia kipato ili uchumi wa nchi uweze kuendelea kukua kwa kasi.

Waziri Mkuu ametembelea maeneo mbalimbali zikiwemo stesheni za SGR, kituo cha treni za mizigo na karakana eneo la Kwala mkoani Pwani, pia amekagua reli, nguzo za umeme pamoja na mitambo ya umeme.

Aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Leonard Chamuriho amesema kazi inayofanyika ni kubwa sana katika kutekeleza mradi huo wa kimkakati wenye urefu wa kilometa 1219 kutoka Dar es Salaam - Mwanza ambapo kipande cha Dar es Salaam - Morogoro tayari kimekamilika kwa asilimia 93 na Morogoro – Makutupora kikikamilika kwa asilimia 70.

“Mhe. Waziri Mkuu ametembelea na kukagua mradi kipande hiki cha kwanza na amejionea mwenyewe maendeleo makubwa yaliyofanyika” alisema Mhe.Chamuriho.

Vilevile, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ameeleza kuwa mahandaki yote yamekamilika asilimia 100, pia madaraja makubwa 51 ambayo yamekamilika zaidi ya asilimia 70 pamoja na makalavati 622.

Pia Ndugu Kadogosa ameongeza kuwa njia zote zenye vivuko vya binadamu na wanyama pamoja na magari zimetengwa ili kuepusha njia ya reli isiwe na uhusiano na shughuli nyingine za kibinadamu kwa sababu za kiusalama.