Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MRADI WA SGR UMEKIDHI VIWANGO; BODI KUTOKA PPRA


news title here
23
June
2023

Shirika la Reli Tanzania limepokea ugeni wa bodi ya wakurugenzi kutoka Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma - PPRA ambapo wamefanya ziara ya siku mbili kutembelea ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa - SGR kutoka Dar es Salama hadi Dodoma hivi karibuni Juni, 2023.

Bodi ya wakurugenzi kutoka PPRA imetembelea mradi wa SGR kwa lengo la kukagua na kujiridhisha juu ya thamani ya fedha iliyotumika kukidhi viwango vinavyotakiwa katika kujenga mradi huo mkubwa wa kimkakati.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi kutoka PPRA Dkt. Leonada Mwagike ameeleza kuwa ujenzi wa mradi wa SGR umekidhi viwango na ubora utakaowezesha usafirishaji wa abiria na mizigo kwa muda mfupi na treni kufika sehemu kwa wakati.

“Tumeona ubora wa ujenzi uliowekezwa katika mradi huu na nimefurahishwa kwakuwa watanzania wengi wana ujuzi wa kuusimamia mradi huu mkubwa” alisema Dkt. Mwagike.

Naye Mtendaji Mkuu kutoka PPRA Bw. Eliakim Maswi alisema kuwa fedha za umma zinatakiwa zitumike kulingana na maelekezo na Sheria iliyopo hivyo maendeleo ya mradi huo unaenda sambamba na thamani ya fedha iliyowekwa na Serikali.

“PPRA jukumu lake ni kukagua na kuona matumizi yaliyotumika yanalingana na thamani ya fedha iliyowekwa, vitu vilivyofanywa katika mradi huu ni vikubwa sana” alisema Bw. Maswi.

Mkurugenzi Mkuu kutoka TRC Ndugu Masanja Kadogosa ametoa shukurani kwa bodi ya wakurugenzi kutoka PPRA kwa kutembelea mradi wa SGR na kuona maendeleo ya mradi pamoja na kujiridhisha katika maeneo mbalimbali.

“Inatoa picha nzuri kwa kile walichokiona kwenye makaratasi na kuhakiki ujenzi uliofanyika hivi sasa, PPRA kwetu ina umuhimu sana kwa maana ya manunuzi tunafuata Sheria za PPRA“ alisema Ndugu Kadogosa.

Naye Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi kutoka PPRA mhandisi Sylvester Mayunga alisema kuwa reli ya kisasa imejengwa kwa viwango na ubora mkubwa kwa kujenga njia iliyonyooka na kudhibiti sehemu korofi zenye maji kwa kupitisha reli kwenye mahandaki.

“Usimamizi umekuwa mzuri na tumeona vitu vingi vipo imara kuanzia mataruma, kuweka vitu vya kudhibiti wizi na hujuma kwenye njia ya reli “ alisema Mhandisi Mayunga.

Mradi wa SGR kipande cha kwanza kutoka Dar es Salaam - Morogoro kimefikia 98.26% na kipande cha pili kutoka Morogoro - Makutupora 94.19%.