Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MRADI WA SGR KIPANDE CHA TANO ISAKA – MWANZA, TRC YAENDELEA KUTWAA ARDHI


news title here
24
December
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la utwaaji ardhi kupisha ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha tano Isaka - Mwanza linalofanyika katika wilaya ya Nyamagana kata ya Mkuyuni mkoani Mwanza hivi karibuni Disemba, 2022.

Zoezi hilo la utwaaji ardhi linaambatana na uhamishaji makaburi ambayo yamepitiwa na mradi wa SGR yaliyopo katika mtaa wa Mkuyuni Sokoni jijini Mwanza ambapo makaburi takribani elfu moja na Mia tano yanahamishwa na kupelekwa katika eneo la Nyashana kata ya Isamilo.

Mhandisi kutoka TRC Bw. Blasius Mwita ameeleza kuwa zoezi hilo linafuata taratibu zote za kisheria na uadilifu katika kazi ili kuhakikisha limefanyika kiusalama kwa kufuata maslahi ya wananchi na taifa.

Taratibu hizo ni pamoja na kushirikisha uongozi mbalimbali utakaohusika wakati wa kufanya zoezi wakiwemo Mkuu wa mkoa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, viongozi wa dini, wataalamu wa afya, mwenyekiti na mtendaji wa mtaa husika, wataalamu wa ardhi na wathamini, polisi kwaajili ya kulinda usalama wa zoezi na raia.

“Zoezi hili linafuata taratibu zote za kisheria lakini pia linafanyika kwa hekima na busara ili kuhakikisha ndugu zetu waliotangulia tunawahamisha kwa amani na salama“ alisema Mhandisi Mwita.

Mhandisi Mwita alieleza kuwa makaburi hayo ni ya imani ya dini ya kiisilamu hivyo wameshirikisha ndugu pamoja na uongozi madhehebu ya dini ya kiisilamu ikiwemo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania - BAKWATA, Sunni pamoja na Shia mkoa wa Mwanza na vilevile kuambatana na mashekhe wakati wa zoezi kwaajili ya kuombea marehemu na kuelekeza hatua mbalimbali zinazofanyika kwa imani ya dini hiyo.

Naye Shekhe kutoka BAKWATA Bw. Juma Marijani amewasihi wananchi kuwa na subira na imani ili kufanikisha zoezi hilo na kusema kuwa kila jambo hupangwa na Mwenyezi Mungu hivyo jambo hilo limepangwa pia kwaajili ya kukuza maendeleo ya nchi.

“Mwenyezi Mungu hua na makusudi yake hivyo naamini jambo hili pia ni bora na lenye faida kwa nchi sababu litaleta maendeleo kwaajili yetu na vizazi vijavyo” alisema Shekhe Marijani.

Hata hivyo mwenyekiti wa mtaa wa Mkuyuni Sokoni Bw. Saidi Issa ameeleza kuwa wananchi wamepokea vyema suala la kuhamisha wapendwa wao ili kupisha ujenzi wa mradi wa SGR katika kipande hicho cha tano cha Isaka - Mwanza na kuridhia kutoa ushirikiano hadi zoezi hilo litakapokamilika.

“Linapokuja suala la maendeleo kwaajili ya nchi lazima kutoa ushirikiano mzuri sababu ni maendeleo yetu sote” alisema Bw. Saidi.

Utwaaji huo wa ardhi ni kwaajili ya kupisha ujenzi wa njia kuu ya reli ya kisasa katika kipande cha tano Isaka - Mwanza ambacho kitakamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa - SGR kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.