Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MKUU WA MKOA WA MWANZA AWAONYA WATAKAOHUJUMU UJENZI WA SGR MWANZA - ISAKA


news title here
02
August
2021

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na kampeni ya uelewa kwa jamii kuhusu mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR Mwanza hadi Isaka.

Kampeni hiyo iliyoanza tarehe 28 Juni, 2021 imewafikia wananchi katika jamii zinazopitiwa na mradi katika wilaya za Kwimba na Misungwi za mkoani Mwanza, Maswa mkoani Simiyu, Shinyanga Manispaa, Shinyanga vijijini, Kishapu na Kahama mkoani Shinyanga.

Kampeni hiyo endelevu kwa sasa inaendelea katika wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza ambapo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi akiambatana na viongozi wa ngazi ya Mkoa, Wilaya na Kata, amehudhuria mkutano wa hadhara wa kampeni ya uelewa katika eneo la Kamanga Feri, Kata ya Nyamagana wilayani Nyamagana.

Eneo la Kamanga ni maarufu jijini Mwanza kwa biashara ya Samaki watokao ziwa Victoria likijumuisha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo ambao wamejitokeza kwa wingi katika mkutano huo wa hadhara.

Akizungumza baada ya mkutano kufunguliwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza amewataka Wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwa ujumla kuchangamkia fursa zinazoambatana na mradi, aidha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ametoa tahadhari kuwa yeyote atakayejihusisha na hujuma dhidi ya mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR serikali haitasita kuwawajibisha kwa mujibu wa sheria.

“Hii ni elimu ya maendeleo kuhusu mradi huu mkubwa kwenye mkoa wetu, fursa ni nyingi katika mradi lazima zianze na sisi, lakini nitoe onyo kwa yeyote atakayehusika kuhujumu mradi, tutafuatilia” alisema Mhandisi Gabriel

Mhandisi Robert Gabriel pia ameeleza kuwa kampeni hii ni mwanzo tu wa ushirikishwaji wa wananchi na kwamba zoezi hili ni endelevu kwa hatua zote za utekelezaji wa mradi.

“Changamoto zote majibu yake ndio hapa, lakini huu sio mkutano wa mwisho kutakuwa na mikutano mingine kama hii mpaka mambo yaeleweke” aliongeza Mhandisi Robert Gabriel.

Kwa upande Mwingine Mhandisi Robert Gabriel amewataka Wanamwanza kuchukua tahadhari zinazoshauriwa na wataalamu dhidi ya virusi vinavyosababisha UVIKO 19 na kuwa ni muhimu kupuuza uzushi na kusikiliza maelekezo ya wataalamu wa afya.

Kampeni ya uelewa kuhusu Mradi Wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa inafanyika huku zoezi la uthamini kwa ajili ya utwaaji ardhi likitarajiwa kuanza hivi karibuni, pamoja na mambo mengine kuhusu mradi, kampeni inatoa elimu kwa wananchi juu ya mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya zoezi la uthamini, utwaaji ardhi na ulipaji fidia.

“Tunawasihi wamiliki wa maeneo husika na wawakilishi wa taasisi kushiriki kikamilifu katika zoezi la uthamini kuanzia katika hatua ya awali ya utoaji elimu, lakini pia kwa hatua hii tunasisitiza pia kuwa ni vyema kumaliza migogoro ya ardhi kabla ya zoezi la uthamini kwani itapelekea kuchelewa kwa malipo ya fidia” alisema Afisa Mwandamizi, Kitengo cha Ardhi – TRC, Bw. Fredrick Kusekwa

Diwani wa kata ya Nyamagana Bw. Bhiku Kotecha ameongeza kuwa kuanza kwa utekelezaji wa Mradi wa SGR Kipande cha Mwanza hadi Isaka kumekata kiu ya Wananyamagana waliokuwa wakiusubiri kwa hamu mradi huo unaotegemewa kuleta mabadiliko makubwa katika uchumi wa mtu mmoja mmoja na mkoa kwa ujumla.

Kampeni hii ya Uelewa kwa jamii kuhusu Mradi wa SGR Mwanza - Isaka, vilevile inalenga kutoa elimu juu ya masuala ya kijamii, mazingira na elimu kuhusu ulinzi na usalama wa Reli, ambapo wataalamu kutoka TRC, mbali na mikutano ya Hadhara hutumia pia vyombo vya habari katika Mikoa husika kufikisha ujumbe kwa jamii husika.