Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MKUU WA MKOA WA ARUSHA AFUNGUA RASMI KAMPENI YA UELEWA KUEPUSHA AJALI RELINI MKOANI HUMO


news title here
11
August
2020

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Idd Hassan kimanta afungua rasmi kampeni ya uelewa kuhusu ulinzi na usalama wa miundombinu ya reli ili kuepusha ajali relini, hafla hiyo imefanyika jijini Arusha hivi karibuni Agosti 2020.

Lengo la Kampeni hii ni kutoa uelewa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari na mikutano ya ana kwa ana katika makazi ya watu, vijiwe vya madereva, mashuleni na katika vituo vya mabasi ili kuepusha ajali relini zinazoweza kupelekea vifo, uharibifu wa mali na miundombinu ya reli kufuatia mpango wa Serikali wa kurejesha safari za treni kati ya Arusha na Moshi.

“Lengo la kikao hiki ni kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambayo ameyatoa kwa Shirika la Reli Tanzania – TRC kuhakikisha mwishoni mwa mwezi huu Agosti treni inafika Arusha kwa kufuata na kuzingatia taratibu zote” alisema Mhe. Kimanta

Mkuu wa mkoa wa Arusha amefungua kampeni hiyo mkoani humo kwa kufanya mkutano na viongozi wa Wilaya, Tarafa, Kata, Mitaa na Vitongoji ambavyo vinapitiwa na reli katika mkoa huo ili kutoa fursa kwa viongozi hao kupata uelewa mpana kuhusu masuala ya ulinzi na usalama wa miundombinu ya reli ili waweze kuwa mabalozi wazuri katika maeneo yao ya uongozi.

Aidha Mkuu wa mkoa amesisitiza kuwa kila mwananchi analo jukumu la kuhakikisha miundombinu ya reli inakuwa salama lakini viongozi wana nafasi kubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu masuala hayo, hivyo viongozi hao wametakiwa kuitisha mikutano katika maeneo yao ya uongozi ili kuhamasisha wananchi kuhusiana na ulinzi wa miundombinu ya reli.

“Sisi wote ambao reli inapita katika maeneo yetu ya kiutawala tuna jukumu la kuipokea treni, na tukilielewa hili na sisi baadae tuitishe vikao kueleza umuhimu wa kutunza miundombinu ya reli, hii reli ni yetu sote” alisema Mkuu wa Mkoa

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wanahabari na timu ya mawasiiano kutoka Shirika la Reli akiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji Ndugu Focus Sahani, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti ajali Relini Mhandisi Maizo Mgedzi na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano Bi. Jamila Mbarouk ambao walitoa elimu kuhusu namna ya kudhibiti ajali relini kwa viongozi hao.

Shirika la Reli linatarajia kurejesha safari za treni kutoka Tanga na Dar es Salaam kuelekea Moshi na jijini Arusha kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyotoa maelekeza ya kurejesha huduma za treni zilizosimama kwa takribani miaka 30 kwa kanda ya Kaskazini, hivyo basi kila mwananchi ana haki ya kupata uelewa kuhusu mambo ya msingi katika usafiri wa reli hususani ya kiusalama ili aweze kutumia huduma hii kwa usalama zaidi.