Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MKUU WA CHUO CHA RELI ATEMBELEA BANDA LA TRC SABASABA


news title here
03
July
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC limepokea ugeni wa Mkuu wa Chuo cha Teknolojia ya Reli - Tabora (TIRTEC) Ndugu Damas Mwajanga alipotembelea banda la TRC lililopo katika viwanja vya maonesho ya 47 ya biashara ya kimataifa - Sabasaba hivi karibuni Julai, 2023.

Ndugu Mwajanga alisema kuwa maonesho ya biashara ya kimataifa yanatoa fursa kwa watanzania kuja kujionea mambo mbalimbali yanayofanywa na mashirika, taasisi na wajasiriamali wa ndani na nje ya nchi.

"Nampogeza sana Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kadogosa kwa kuruhusu wafanyakazi wa kada mbalimbali kushiriki katika maonesho haya ,kwani watanzania wanashauku ya kujua maendeleo ya mradi wa kimkakati wa reli ya kisasa -SGR " alisema Ndugu Mwajanga

Pia Ndugu Mwajanga alieleza kuwa chuo cha teknolojia ya reli ni chuo kikongwe kilichoanzishwa mwaka 1947 wakati wa ukoloni kikitoa mafunzo mbalimbali ya usafirishaji kwa njia ya reli, hata hivyo Ndugu Mwajanga alisema kuwa chuo hicho kwa sasa kimeboreshwa na kutoa mafunzo ya kozi mbalimbali za usafirishaji kwa njia ya reli kutokana na mabadiliko ya teknolojia.

"Tarehe 26 Juni, 2023 tumekutana na wadau wa usafirishaji na kujadili mitaala mipya ya mafunzo ya usafirishaji kwa njia ya reli ikiwemo kozi ya mafunzo ya SGR na kozi ya uchumi ili kupata wataalamu wa kuboresha biashara katika sekta ya usafirishaji kwa njia ya reli, kozi hizi zitaanza mwaka huu 2023" alisisitiza Ndugu Mwajanga.

Mkuu wa kitengo cha habari na uhusiano kutoka TRC Bi. Jamila Mbarouk amesema watanzania watakao tembelea banda la TRC kwenye maonesho ya sabasaba watapata fursa ya kuelezewa historia ya TRC ilipotoka, ilipo na inapoelekea kwenye mageuzi ya usafirishaji kwa kutumia treni ya kisasa yenye viwango vya kimataifa.

"Ukiwa katika banda la TRC utakutana na mtaalamu kutoka chuo cha teknolojia ya reli utapewa maelezo ya chuo na wanaohitaji kujiunga na chuo hicho watapewa fomu za kujiunga na chuo" alisema Bi.Jamila.

Maonesho ya 47 ya biashara ya kimataifa yenye kaulimbiu isemayo "Tanzania mahali sahihi kwa biashara na uwekezaji" yameanza rasmi mnamo tarehe 28 Juni, 2023 na yatahitimishwa tarehe 13 Julai, 2023.