Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MKURUGENZI MKUU WA SHIRIKA LA RELI TANZANIA AFUNGUA BARAZA LA PILI LA WAFANYAKAZI


news title here
15
February
2020

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania – TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amefungua Baraza la pili la Wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania katika ukumbi wa ‘Fire and Safety’ uliopo Bandari jijini Dar es Salaam Februari 15, 2020.

Baraza la Wafanyakazi TRC hukutana kila mwaka kwa lengo la kujadili masuala tofauti yanayohusu Shirika ikiwemo, utendaji, mafanikio, changamoto lakini pia Baraza hili huweka maadhimio na kujadili bajeti ya Shirika kabla ya kwenda Wizara ya Fedha na Mipango, ambapo tangu kuanzishwa upya kwa Shirika la Reli mwaka 2018 hili ni Baraza la pili la wafanyakazi kufanyika.

Baraza la wafanyakazi TRC ni kama bunge la wawakilishi wa Wafanyakazi kwani huwakilisha na kuwasilisha mada mbalimbali zinazohusu Shirika na Wafanyakazi moja kwa moja kwa kuongelea Mapito ya Shirika, Ufanisi, Kuboresha, kutoa majibu ya maswali, maelekezo, mawazo mapya, na namna ya kutatua Changamoto, mipango ya Shirika kwa miaka ijayo kwahiyo Baraza hili ni muhimu sana kwa Shirika“aliongea Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Ndugu Masanja Kungu Kadogosa.

Akiongea na Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi TRC mweyekiti wa Baraza hilo Ndugu Masaja Kungu Kadogosa amesisitiza Ushirikiano na uwazi katika mambo yanayojadiliwa ili Shirika liweze kukua Zaidi kwa kuboresha na kutatua au kupunguza changamoto za Shirika ili kufikia malengo yaliyopangwa.

Aidha Mwenyekiti wa Baraza hilo alipata fursa ya kutoa taarifa fupi ya utendaji wa Shirika kwa mwaka 2019 na kuonesha kuwa Shirika limefanikiwa kuendelea kusimamia miradi yake ambayo ni Ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR, Mradi wa Uboreshaji wa Reli ya Kati – TIRP, Ukarabati wa Behewa, Ufufuaji wa Reli za zamani ambazo ziliacha kufanya kazi

Katibu wa Baraza la wafanyakazi TRC Bwana Edwin Kalisa amesema kuwa Baraza la wafanyakazi linajadili masuala tofauti yanayohusu maendeleo ya Shirika hasa Bajeti ambayo ni muongozo wa Shirika katika mipango na utendaji hasa katika kipindi hiki ambacho Shirika linasimamia miradi mikubwa ikiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya Kisasa, ukarabati wa reli ya kati – TIRP, ufufuaji wa reli za zamani na ukarabati wa behewa.

“Bila kukaa, kujadili na kuona ujenzi unaendeleaje hatutaweza kufahamishana kuhusu mradi tunaousimamia, chini ya uongozi wa awamu ya Tano wa Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya watanzania wote, wajumbe wa Baraza ni wawakilishi wa wafanyakazi TRC nchi nzima kutoka kanda, wilaya, hivyo ni kama mkutano wa wafanyakazi wote Tanzania kwa sababu tunatunga sera za Shirika” alisema Kalisa

Naye Bi. Elizabeth Msemwa kwa niaba ya Msemaji wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania – TRAWU ameupongeza na kuushukuru uongozi wa Shirika la Reli nchini kwa mafanikio yaliyopatikana katika huduma, miradi na kujali maslahi ya wafanyakazi wa TRC na kuongeza kuwa jitihada za ziada zinapaswa kuchukuliwa ili kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi ili kwenda sambamba na mabadiliko yanayoendelea ndani ya shirika.