Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MKURUGENZI MKUU TRC AZINDUA RASMI MFUMO WA MASIJALA MTANDAO


news title here
14
April
2020

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amezindua mfumo wa kidigitali wa Masijala Mtandao (E - Filling) katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya maka Makuu TRC jijini Dar es Salaam Aprili 14, 2020.

Mfumo huo wa kisasa utarahisisha shughuli za kila siku za Shirika katika kutuma, kupokea na kuhifadhi kumbukumbu za nyaraka za Shirika na Serikali kwa njia ya kielektroniki. Vile vile mfumo huu utasaidia kupunguza muda uliokuwa unatumika katika kuwasilisha nyaraka kutoka ofisi moja hadi nyingine au taasisi moja kwenda nyingine.

Aidha, mbali na vita inayoendelea ya kupambana na Ugonjwa wa Corona zoezi hilo limefanyika kwa tahadhari ambapo ni wajumbe wachache wa Menejimenti ya TRC walihudhurua zoezi hilo huku Mganga Mkuu wa Shirika akiwaongoza wajumbe kunawa mikono na kuvaa Barakoa ili kuhakikisha kila mmoja anajikinga na maambukizi ya ugonjwa huo

Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Kadogosa amesama kuwa mfumo huo ni wa muhimu sana hasa katika taasisi za serikali kwa kusaidia kutokomeza upotevu wa nyaraka za serikali katika Shirika, kuimarisha ulinzi wa nyaraka pamoja na kudumisha ubora wa kazi kwa kuhakikisha nyaraka zote zinafanyiwa kazi kwa wakati. Lengo ni kuweka uzoefu kwa watu kutumia mfumo huo wa masijala mtandao na kusaidia kupunguza msongamano wa watu wanaotoka na kuingia hasa katika kipindi hiki cha kuzuia mkusanyiko wa watu kutokana na janga la virusi vya Corona.

“Mimi sitapitisha nyaraka ambayo haitakuwa katika mfumo huu wa ‘E – File’’, alisema Ndugu Kadogosa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa – Ofisi ya Rais Bw. Gaspar Kileo amesema kuwa amefurahishwa sana na ushirikiano wa Shirika la Reli kwa kufanya kazi pamoja kuboresho mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu katika taasisi hiyo ya reli na mfumo huo mpaka sasa upo kwenye vision ya tatu ya mfumo.

“Tumepata ushirikiano mkubwa hadi hapa tulipofikia na wakati wowote tupo tayari kutoa ushirikiano endapo zitajitokeza changamoto za hapa na pale”, alisema Bw. Kileo.

Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala Bi. Amina Lumuli ambaye ni mdau mkubwa wa mfumo huo amesema kuwa mfumo huu wa Masijala mtandao utarahisisha kazi nyingi huku majukumu mengine yakiendelea na vilevile kuona nyaraka kwa uharaka na kupunguza upotevu wa nyaraka unaojitokeza mara kwa mara.

“Mfumo huu ni rafiki utatuwezasha kupunguza nyaraka za karatasi na nina imani utaturahisishia sana kazi”, alisema Bi. Amina.