Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MKURUGENZI MKUU TRC ATOA NENO LA SHUKURANI, AONESHA JARIDA LA RELI NA MATUKIO 2021


news title here
26
January
2022

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania – TRC Masanja Kadogosa amekutana na waandishi wa habari na kutoa neno la shukurani kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wa TRC kwa Wananchi, Vyombo vya Habari, Wateja pamoja na wadau wengine wa usafiri wa reli kwa ushirikiano katika kutimiza majukumu ya Shirika, Januari 26, 2022.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania emeeleza baadhi ya mafanikio ya Shirika kwa mwaka 2021 ambapo mapato yalipanda kwa 29% kutoka Bilioni 33 hadi Bilioni 49 kufuatia uboreshaji wa njia, ukarabati wa behewa, ununuzi wa vichwa na behewa mpya bamoja na maboresho makubwa ya utoaji huduma yaliyofanyika kwa mwaka 2021.

Kadogosa ameongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuliwezesha Shirika kifedha kwajili ya kutekeleza majukumu yake ikiwemo utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa awamu ya Kwanza Dar es Salaam – Mwanza yenye vipande vitano ambavyo ni Dar es Salaam - Morogoro chenye jumla ya urefu wa km 300, Morogoro - Makutupora chenye jumla ya urefu wa km 422, Makutupora - Tabora chenye jumla ya urefu wa km 368, Tabora - Isaka chenye jumla ya urefu wa km 163 na Isaka - Mwanza chenye jumla ya urefu wa km 341.

“Hivi sasa Serikali kupitia TRC inatekeleza vipande 4 ambavyo ni Dar es Salaam – Morogoro ambacho kimefika 95%, Morogoro – Makutupora ambacho kimefika 79%, Mwanza – Isaka ambacho kimefika 4% pamoja na kipande cha Makutupora – Tabora kikiwa katika hatua za awali mara baada ya mkataba wake kusainiwa hivi karibuni Disemba 2021 na hivi karibuni Shirika linatarajia kuweka jiwe la msingi kuashiria kuanza ujenzi” alisema Kadogosa

Aidha, katika mkutano huo Kadogosa alipata fursa ya kuonesha toleo maalumu la mwaka 2021 la Jarida la Reli na Matukio ambalo lina taarifa na matukio makubwa na muhimu ambayo yametokea kwa kipindi cha mwaka kuanzia Januari hadi Disemba 2021 kwa lengo la kuuhabarisha umma na kutunza kumbukumbu za TRC.

“Tunahimiza sana wananchi kufuatilia yale yanayotokea katika reli ukizingati tuna mradi mkubwa wa ujenzi wa reli wenye thamani ya Shilingi Trilioni 14.7, kwahiyo huu ni mradi mkubwa sana kwa serikali hivyo tumekabidhiwa dhamana kuhakikisha tunawahabarisha wananchi wajue fedha zao zinakwenda wapi” aliongeza Kadogosa

Kadogosa alisema kuwa “Mpaka sasa tumeagiza vichwa na behewa ambavyo vitatumika katika uendeshaji wa reli ya kisasa ambazo zinatarajiwa kufika nchini Tanzania mwishoni mwa mwezi Aprili 2022”. Kadogosa amesisitiza kuwa kuchelewa kwa Behewa na vichwa hivyo ni kutokana na uwepo wa changamoto ya UVIKO19 ambayo imepelekea kupungua kasi ya uzalishaji katika nchi zinazozalisha vichwa na Behewa hizo.

Ndugu Kadogosa alimaliza kwa kuwasihi wananchi na wadau kuendelea kutoa ushirikiano katika kulinda miundombinu ya reli kwa manufaa ya Taifa, kuzingatia alama za usalama wa reli pindi wanapokuwa katika makutano ya reli na barabara ikiwemo kusimama umbali salama kutoka katika makutano ya reli na barabara kuchukua tahadhari pindi wanapokatiza reli.