Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MKURUGENZI MKUU TRC AMESHIRIKI MKUTANO WA WAHASIBU NA WAKAGUZI WA HESABU TANZANIA


news title here
03
December
2020

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la reli Tanzania - TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ameshiriki katika mkutano mkuu wa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu za Serikali na kuwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi wa ujenzi wa reli kisasa - SGR katika mkutano wa mwaka wa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa APC, Bunju jijini Dar es Salaam, Disemba 03, 2020.
Aidha, mkutano huo uliobeba ujembe wa uhasibu ni nguzo mhimu katika utawala bora umekuwa na lengo la kuwakutanisha Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu nchini ili kukutana na kufanya tathimini ya mafanikio na changamoto kwa mwaka mzima na mipango ya baadae kwa mwaka unaofuatia.
Mkurugenzi Mkuu amewasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam mpaka Makutupora Singida ambapo anasema mradi huu ni mkubwa hivyo hauwezi ukatekelezwa bila kuhusisha wataalam wa kada ya uhasibu na wakaguzi wa hesabu za Serikali.
“Tunapozungumzia utawala bora katika Taasisi za Umma hatuwezi kuachanisha fani ya uhasibu na ukaguzi wa fedha, kwa hiyo ni mkutano wenye tija na ni watu ambao ni mhimu sana kwa Shirika na kwa mradi wa SGR. mtakuja kesho kutembelea mradi ili muweze kuona kile ambacho nimewasilisha, huku mkiangalia gharama iliyotumika na kazi inayoendelea kufanyika” alisema Mkurugenzi Mkuu TRC.
Kwa upande wake Francis Mwakapalila ambaye ni Mhasibu Mkuu Wa Serikali ambaye katika Mkutano amemwakilisha Mgeni Rasimi Waziri wa fedha na mipango, Dkt Philip Mpango. Mhasibu Mkuu wa Serikali ameeleza uhusiano uliopo kati ya taaluma ya uhasibu na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa unaosimamiwa na Shirika la reli Tanzania ambapo amebainisha kuwa wahasibu wanahusika kikamilifu katika mradi huu kwa kuwa wao ndio wanaotoa hesabu ya rasilimali inayotumika katika ujenzi wa reli ya kisasa.
“Suala la Reli ya Kisasa ni agenda kubwa katika mkutano huu kwa sababu katika swala la kukua kwa uchumi wa nchi hatuwezi kuacha kutaja Reli ya kisasa na ni rasilimali kubwa ya nchi imetumika hapo na wanaotoa hesabu ya rasilimali hiyo ni wahasibu hivyo huwezi kuongelea reli bila wahasibu ambao wanatoa hesabu ya rasilimali iliyotumika” alisema Mhasibu Mkuu wa Serikali.
Katika hatua nyingine, mkutano huu umekwenda sambamba na Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kungu Kadogosa kupewa zawadi kama sehemu ya kutambua mchango wake kwa kushiriki mkutano huu sanjari na kuwasilisha taarifa ya ujenzi wa Reli ya kisasa - SGR.