Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MKURUGENZI MKUU TRC AKUTANA NA BALOZI WA RWANDA KUJADILI MRADI WA SGR ISAKA - KIGALI


news title here
08
October
2021

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania – TRC Masanja Kadogosa akutana na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania Meja Jenerali Charles Karamba na kujadili kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR Isaka – Kigali, mazungumzo hayo yamefanyika katika ofisi ya Mkurugenzi Mkuu TRC jijini Dar es Salaam, Oktoba 05, 2021.

Shirika la Reli Tanzania linaendelea na utekelezaji wa mradi wa SGR awamu ya kwanza Dar es Salaam – Mwanza yenye jumla ya vipande vitano, Dar es Salaam – Morogoro, Morogoro – Makutupora, Makutupora – Tabora, Tabora - Isaka na Isaka – Mwanza, aidha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TRC imeweka mkakati wa kuhakikisha reli ya SGR inajengwa na kuzifikia nchi jirani ikiwemo Rwanda.

Mkutano uliofanyika kati ya Balozi Major Jenerali Charles na Mkurugenzi Mkuu Masanja Kadogosa ulilenga hasa kujadili jinsi mradi wa reli ya kisasa Isaka – Kigali utatekelezwa ikiwemo kuona namna ya kupata fedha za kutekeleza mradi huo lakini pia ushirikiano wa nchi hizo katika kubadilishana uzoefu kwa wataalamu watakaofanya mradi huo.

“Lengo la kuja ni kuhusu namna tutakavyofanya hii kazi, fedha zitatoka wapi na itafanyika namna gani na kingine ni kwamba, Tanzania imeenda mbali kuna kazi ambayo imefanyika kutoka hapa Dar es Salaam hadi Morogoro na wamefikia 95 na kuna kazi nyingine inafanyika Morogoro Makutupora na Mwanza - Isaka na sisi tutaanzia Isaka hadi Kigali” alisema Major Jenerali Charles

Balozi Meja Jenerali Charles amebainisha baadhi ya faida ambazo nchi ya Rwanda itazipata kupitia reli hiyo itakayojengwa kutoka Isaka hadi Kigali Rwanda kwamba itakwenda kupunguza muda wa safari pamoja na bei za bidhaa nchini kwao

“Reli itatusadia kupunguza muda wa kusafirisha mizigo pia itapunguza bei, sio Rwanda peke yake, tutapitia Rwanda hadi Jamhuri ya Kongo” alisema Meja Jenerali Charles

Akifafanua kuhusu mkakati wa kushirikiana kuhusu wataalamu pamoja na namna walivyojiandaa katika kuwatumia wanyarwanda katika kutekeleza mradi huu kama inavyofanyika hapa nchini, Balozi Meja Jenerali Charles ameeleza kuwa wamejipanga kuleta wataalamu kushiriki katika mradi wa SGR unaoendelea kutekelezwa kwa lengo la kujifunza na kuwaongezea uwezo.

“Tuna njia mbili ambazo tunataka tujaribu ili wataalamu wetu wapate ujuzi, njia ya kwanza ni kuleta wataalamu kufanya kazi hapa Tanzania lakini pia ni kuleta vijana wadogo kujifunza chuoni pale Tabora ili tukianza kujenga ya kwetu kutokana na ujuzi na watalaamu tutakaowapata kutoka hapa Tanzania watatumika katika ujenzi huo wakishirikiana na wataalamu wa Tanzania” alisema Meja Jenerali Charles

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa ameushukuru ugeni huo na kusema kuwa mkutano huo ni kwa ajili ya kujadili maagizo ya Marais wa nchi hizo, Tanzania na Rwanda juu ya ujenzi wa reli ya kisasa itakayoziunganisha nchi hizo mbili.

“Namshukuru Mhe. Balozi kwa kututembelea na haya tuliyazungumza tukiwa Rwanda na ni maagizo ya Marais wawili Mhe. Paul Kagame na Samia Suluhu Hassan, walipokutana walikubaliana vitu vingi lakini kimoja wapo ni ushirikiano wa ujenzi wa reli kutoka Isaka kwenda Rusumo, Kigali na njia ya uwanja wa ndege wa Kigali” alieleza Kadogosa