MKATABA WA UNUNUZI WA BEHEWA 1430 ZA MIZIGO ZA RELI YA KISASA – SGR WASAINIWA
February
2022
Shirika la Reli Tanzania – TRC limesaini mkataba na kampuni ya CRRC International kutoka nchini China kwaajili ya ununuzi wa Behewa 1430 za mizigo zitakazotumika katika reli ya kisasa – SGR, hafla ya utiaji saini imefanyika katika ukumbi wa mikutano makao makuu TRC Februari 08, 2022.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa Serikali na Shirika, ambapo Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ameshuhudia zoezi la utiaji saini maa baada ya kupata taarifa fupi ya mkataba wa ununuzi wa behewa hizo pamoja na maendeleo ya ujenzi wa reli ya kisasa nchini kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa kuwa Ujenzi wa reli ya kisasa unaoendelea kwa sasa ni kipande cha Dar es Salaam – Morogoro umefika 95%, Morogoro – Makutupora umefika 81% na Mwanza – Isaka umefika 4%.
Hata hivyo Waziri Mbarawa alisema kuwa katika Behewa hizo 1430 zitakazotengenezwa zipo Behewa 60 za mifugo ambapo Behewa moja itakuwa na uwezo wa kubeba takribani Ngo’mbe 100 ambayo ni sawa na Ngo’mbe 6,000 kwa Behewa 60. Pia zipo behewa 50 maalumu kwa ajili ya kubeba magari ambapo behewa moja itakuwa na uwezo wa kubeba magari madogo 8 ambayo ni sawa na magari 400 kwa behewa 50.
Mhe. Waziri alifafanua kuwa “kutokana na uwezo mkubwa wa reli ya kisasa, behewa hizi zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mrundikano wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam ambapo treni moja itakuwa na uwezo wa kubeba Tani 10,000 kwa mkupuo ambayo ni sawa na malori 500” alisema Prof. Mbarawa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri aliwapongeza wafanyakazi wa Shirika la Reli kwa usimamizi mzuri wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa na kuwaomba waendelee kuchapa kazi kwa kutumia weledi walionao na jitihada ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuhudumia wananchi na kukuza uchumi wa Taifa.
Mkurugenzi Mkuu TRC, Ndugu Masanja Kadogosa katika taarifa yake amesema kuwa,
“Mkataba huu ni wa ununuzi wa Behewa 1430 za mizigo za reli ya kisasa ambao unagharimu Dola za Kimarekani Milioni 127.2, ni mkataba wa miezi 12 yaani mwaka mmoja utakaohusisha usanifu na utengenezaji wa Behewa kwaajili ya kubeba mizigo ya aina mbalimbali kulingana na aina ya behewa na matakwa ya mteja kupitia reli ya kisasa”.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi mkuualiweka wazi kuwa aina ya behewa zitakazonunuliwa kupitia mkataba huu ni, Behewa 600 aina CCB (Container Carrier Bogie) kwaajili ya kubeba makasha, Behewa 400 aina ya CLB (Covered Large Bogie) kwaajili ya kubeba mizigo ya jumla ikiwemo Sukari, Saruji, Chumvi, Pamba, Tumbaku na Kahawa, Behewa 190 aina ya PTB (Petroleum Tank Bogie) kwaajili ya kubeba mafuta aina zote, Behewa 70 aina ya HLB (High Large Bogie) kwaajili ya Mabomba, Mbao, Magogo na Vyuma, Behewa 50 aina ya MGB (Motor Goods Bogie) kwaajili ya kubeba magari na Behewa 50 aina ya CWB (Cattle Wagon Bogie) kwaajili ya kubeba Ng’ombe.
Kwa upande wake Mwakilishi wa kampuni ya CRRC ambaye ni Meneja Msaidizi Bw. Tang Yun Pengamesema kuwa “Leo ni siku nzuri kwetu CRRC kwa sababu haikuwa rahisi kufikia hapa, nakumbuka mwaka jana tulishiriki katika mradi wa uboreshaji wa reli ya kati, hivyo tuna ujasiri wa kutosha kusanifu na kutengeneza behewa bora na imara kwaajili yenu” alisema Bw. Peng.
Shirika la Reli Tanzania linatarajia kukamilika kwa manunuzi na kuwasili kwa behewa hayo mapema Februari 2023 ambako kutakwenda sambamba na kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha pili Morogoro – Makutupora ambacho kwa umbali huo kutaweza kuleta tija na faida katika uendeshaji wa huduma ya usafirishaji mizigo.