MIAKA 3 MFULULIZO SHULE YA MSINGI ITIGI RELI YAWA KINARA KITAALUMA

October
2022
Shule ya Msingi Itigi Reli inayosimamiwa na Shirika la Reli Tanzania – TRC iliyopo wilaya ya Manyoni mkoa wa Singida imefanya mahafali ya 28 ya darasa la saba mkoani Singida, Oktoba 8, 2022..
Shule ya Msingi Itigi Reli (Bweni) ilianzishwa mwaka 1987 ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa watoto wa wafanyakazi wa Shirika la Reli wanaofanya kazi katika maeneo ambayo hakuna shule za msingi ama shule ziko mbali na maeneo wanayofanyia kazi.
Hata hivyo TRC inaendelea kuwahudumia wanafunzi 66 waliohitimu shule ya msingi Itigi Reli na kupangiwa shule za sekondari za kutwa za kata kwa kuwapatia malazi na chakula.
Kwa sasa shule ina jumla ya wanafunzi 136 ambapo wanafunzi 37 wamehitimu darasa la saba mwaka 2022.
Mgeni Rasmi, Bi. Amina Lumuli, Mkurugenzi wa Rasilimari Watu na Utawala TRC alianza kwa kupongeza walimu kwa kazi kubwa ya kutoa elimu bora na usimamizi na kuifanya shule ya Itigi kufaulisha wanafunzi wote kwa takribani miaka mitatu mfululizo, kwa upande mwingine amewaasa wanafunzi na wahitimu wakaendeleze stadi za kazi ambazo wamekuwa wakijifunza shuleni, kuwa wanye adabu, utii na heshima kwa jamii pamoja na kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kwa kujiepusha na vitendo viovu.
Katika hatua nyingine Mgeni rasmi ameahidi menejimenti ya TRC kushirikiana katika kutatua changamoto mbalilmbali ambazo zinawakumba wanafunzi katika masomo, walimu katika utendaji kazi na wafanyakazi katika kutimiza majukumu ya kila siku shuleni hapo.
Naye Mwalimu Mkuu Bi. Grace Gyuda alibainisha kuwa Shule imekuwa ikifanya vizuri katika ngazi ya kata, wilaya na hata mkoa kwa miaka mitatu mfululizo.
Vilevile Mwalimu Mkuu amewaeleza wazazi kuwa wahitimu wana ndoto kubwa ambazo wazazi wana nafasi kubwa ya kuwasikiliza na kuhakikisha ndoto zao zinatimia.
Katika risala ya Shule ya iliyowasilishwa na walimu kwa mgeni rasmi ilieleza mafanikio ya kitaaluma kwa miaka mitatu katika mitihani ya ndani na nje ya shule.
“Kwa miaka mitatu shule hii imekuwa katika nafasi nzuri sana kwa mwaka 2019 katika wilaya ilishika nafasi ya 2 kati ya 18, mkoa ilishika nafasi ya 8 kati ya 375 na kitaifa nafasi ya 655 kati ya 9929 ikiwa ufaulu ni 100%. Kwa mwaka 2020 kiwilaya ilikuwa 1, mkoa ilikuwa ya 4, kitaifa ilikuwa ya 522 ikiwa ufaulu ni 100%. Mwaka 2021 kiwilaya ilikuwa ya 1, mkoa ya 8, kitaifa 738 ikiwa ufaulu ni 97%” aliseama Mwalimu Nyanda.
Kwa upande wake Mwakilishi wa wazazi, Bi Tilfely Yotam alitoa nasaha kwa wahitimu kwa kuanza kuwashukru walimu kwa malezi bora ya elimu na dini tangu walipoingia darasa la kwanza na leo wakiwa wanahitimu hata hivyo aliwaasa wahitimu na wanafunzi wanaobaki kuzingatia elimu maana ndio uzima na ufunguo wa maisha ya sasa na baadaye..
Nao wahitimu katika risala yao kwa Mgeni Rasmi, walilishukuru Shirika la Reli kwa kuwapa fursa ya kusoma katika shule ya Itigi Reli na kupata elimu bora, na kufanya vizuri katika mitihani ya ndani, kata, wilaya na mkoa. wahitimu waliliomba Shirika la Reli Tanzania kuwaongezea vifaa vya kujifunzia pamoja na vifaa vya michezo kwani wamekuwa wakishiriki katika michezo katika ngazi ya mkoa.