MHE. KASEKENYA; WAZAWA ZAIDI YA 1000 KUPEWA KIPAUMBELE CHA AJIRA MRADI WA SGR
December
2021
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya amefanya ziara ya kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha kwanza kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam Disemba 22, 2021.
Lengo la ziara hiyo ni kuona maendeleo ya mradi wa SGR na kujiridhisha kuwa sehemu kubwa ya ujenzi imekamilika.
Mhe. Kasekenya alisema kuwa zaidi ya watu 1000 watapewa dhamana ya kusimamia reli ya SGR ambapo hadi sasa ajira zimeanza kutolewa kwa awamu ambapo zaidi ya watu 300 tayari wapo kwenye mchakato wa kuajiriwa ili kufanya kazi katika reli hiyo ya kisasa.
“Watanzania ambao mmepata bahati ya kuwa sehemu ya huu mradi taifa linawategemea kusimamia vyema na kuendesha treni” alisema Mhe. Kasekenya.
Mhe. Kasekenya ameeleza kuwa mradi wa SGR umekamilika kwa asilimia 95 kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro na asilimia 5 ambazo hazijakamilika ni barabara inayounganisha reli na bandari, madaraja matatu yaliyopo eneo la Vingunguti na Karakata ambapo viko mbioni kukamilika.
Aidha Mhe. Kasekenya ameeleza kuwa pamoja na changamoto mbalimbali zinazojitokeza kutokana na mlipuko wa ugonjwa hatarishi wa UVIKO19 ambao unasababisha baadhi ya vifaa vya ujenzi kutofika nchini kwa wakati, pia amewaasa viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia mradi huo wa SGR kuendelea kusimamia kwa ukaribu wakandarasi wanaojenga reli ili mradi uweze kukamilika kwa haraka zaidi.
“Watanzania wanahitaji kuona treni ya kisasa ikitembea” alisema Mhe. Kasekenya.
Pia Mhe. Kasekenya alisema kuwa majaribio yataanza kufanyika mapema ili kujiridhisha kuwa treni hiyo itafanya kazi kwa ufasaha bila visingizio kwakuwa reli hiyo inaweza kutumika na treni ya umeme pamoja na treni zenye uwezo wa kutumia mafuta aina ya Dizeli.
Naye Meneja Mradi wa SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro Mhandisi Simon Mbaga amesema kuwa mradi wa SGR upo katika hatua za mwisho za ujenzi ambapo kazi kubwa ambayo imesalia ni kazi ya ujenzi wa uzio ambayo iko mbioni kukamilika na kuwa tayari kuanza majaribio ya kuendesha treni ya umeme.
“Mradi mpaka sasa unaendelea vizuri pamoja na changamoto zote zinazojitokeza ila ujenzi haujawahi kusimama” alisema Mhandisi Mbaga.
Hata hivyo Mhandisi Mbaga alisema kuwa watanzania wengi watarajie kupata ajira hasa katika huduma za uendeshaji wakiwemo wahandisi, mafundi na watu wenye fani mbalimbali ambapo serikali itatoa kipaumbele hasa kwa vijana ili kuzidi kukuza uwezo na uzoefu kwa vijana wa kitanzania.
“Mradi huu utafanya idadi kubwa ya watu kupata ajira hivyo ni jukumu letu kuutunza, kuuthamini na kuendelea kuchapa kazi kwa faida yetu na nchi” aliongezea Mhandisi Mbaga.
Mradi wa SGR ambao ujenzi wake una vipande vitano kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza utaleta faida kubwa nchini kwa wananchi kupata ajira, kukua kwa biashara pamoja na sekta ya usafirishaji kwa njia ya reli.