MAKAMANDA, MAAFISA WANAFUNZI JWTZ WATEMBELEA SGR MWANZA – ISAKA KATIKA ZIARA YA KIMAFUNZO

October
2022
Makamanda na maafisa wanafunzi kutoka chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha JWT Duluti, Arusha, wakiongozwa na mkuu wa Chuo hicho Brig. Gen. Sylvester Ghuliku wametembelea kipande cha tano cha Mradi wa ujenzi wa SGR Mwanza – Isaka, 13 Oktoba, 2022.
Pamoja na wakufunzi kutoka chuo hicho ziara pia ilihusisha maafisa wanafunzi kutoka nchi mbalimbali Barani Afrika zikiwemo, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Afrika ya Kusini, Nigeria, Misri, Eswatini, Msumbiji na Malawi, aidha kundi lilijumuisha Maafisa wanafunzi kutoka nchini India.
Brig. Gen. Ghuliku ameeleza kuwa lengo la ziara ni sehemu ya mafunzo ya Maafisa wanafunzi yaliyobeba dhana ya “Amani na Usalama kwa Maendeleo Endelevu”.
“Tunawaleta wanafunzi ili kujionea maendeleo ya nchi yetu, walio wengi kati yao wanatoka ukanda wa Afrika Mashariki kwahiyo wanajionea hatua iliyopigwa na watakaporudi kwenye nchi zao, wajue kitu gani kinaendelea Tanzania na wao watafanya kulingana na maendeleo haya” aliongeza Brig. Gen. Ghuliku.
Kwa upande wa TRC, Mhandisi Blasius Mwita ameeleza kuwa ziara hiyo ni muhimu kwa kuwa Amani ni moja ya kiungo muhimu katika utekelezaji wa mradi.
Mhandisi Mwita, aliongeza kuwa ujenzi wa SGR Kipande cha Mwanza – Isaka chenye urefu wa KM 341 unaendelea vizuri ambapo mpaka sasa maendeleo ya ujenzi yamefikia zaidi ya 14% mbapo ujenzi wa tuta, madaraja, makaravati na vivuko pamoja na utandikaji wa mkongo wa mawasiliano ya reli, zkiwa ni miongoni mwa kazi zinazoendelea.
Kwa upande wao maafisa wanafunzi katika ziara hiyo wameelezea kushuhudia maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika ujenzi wa reli kipande cha Mwanza – Isaka, huku wakiitaja miundombinu hiyo ya kisasa kama kichocheo cha ushirikiano kati ya nchi za Afrika Mashariki na Ukanda wa SADC.
“Reli hii itatusaidia wote, watu wa Afrika Mashariki na eneo la SADC hasa katika sekta ya biashara kupitia usafirishaji rahisi na nafuu” alisema Meja. Peter Sebyiga kutoka Tanzania.
Aidha, Luteni Kanali. Evance Kuzakuza kutoka Malawi amesema kuwa“ aina hii ya miradi inanyanyua ushirikiano kati ya nchi kwa ukanda mzima, mfano sisi Malawi tunaitegemea sana Bandari ya Dar es Salaam, kwahiyo mpango wa kuifikisha reli ya kiwango hiki katika mpaka wa kusini mwa Tanzania itainua sana kibiashara kati ya nchi zetu mbili.
Ziara ya makamadna na Maafisa wanafunzi kutoka chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha JWT Duluti, Arusha imefanyika wakati ambapo Shirika la Reli Tanzania linaendelea na awamu ya pili ya Kampeni ya Uelewa kwa jamii kuhusu ujenzi wa SGR kipande cha Mwanza – Isaka, ambapo tayari kampeni hiyo imefanyika wilayani Shinyanga vijijini na kufikia Shinyanga Halmashauri, huku ikitegemewa kuifikiwa mikoa ya Simiyu na Mwanza.