Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MAKABURI TAKRIBAN 228 WILAYANI MASWA MKOA WA SIMIYU KUPISHA UJENZI WA RELI YA KISASA - SGR


news title here
21
October
2021

Shirika La Reli Tanzania - TRC limendelea na zoezi la uhamasishaji wananchi kuhusu zoezi la uhamishaji makaburi ili kupisha ujenzi wa reli ya kisasa - SGR wilayani Maswa mkoa wa Simiyu hivi karibuni Oktoba, 10, 2021.

Katika zoezi hilo takribani makaburi 228 yanatarajiwa kuhamishwa katika vijiji sita (6) ambavyo ni vijiji vya Gulung’washi ambayo kuna jumla ya makaburi 132, Kijiji cha Lali makaburi 12, Kijiji cha Muhida makaburi 54, Kijiji cha Nyashimba 27, Kijiji cha Bugolo makaburi 2 na Bukigi kaburi 1.

Zoezi hilo la uhamasishaji wanachi lilianzia ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Maswa kwa kufanya kikao maalumu cha namna ya utekelezaji wa zoezi hilo kati ya Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mheshimiwa Aswege Enock Kaminyonge na Timu ya Maafisa kutoka Shirika la Reli Tanzania ambao wapo Wilayani hapo.

Akizunguza katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Maswa amelipongeza Shirika La Reli Tanzania kutekeleza zoezi la uhamishaji makaburi kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu kitu ambacho kimesaidia kuondoa migogoro na malalamiko kutoka kwa wanachi wa Wilaya hiyo.

“Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana kwa ushirikiano wenu, kazi imefanyika vizuri hatujapata malalamiko kuhusiana na uthamini wenu wa maeneo naamini elimu ambayo mmeitoa mliifikisha vizuri kwa wananchi na mikutano ile nafikiri wananchi waliielewa, hatujapata shida“ alisema Mheshimiwa Enock Kaminyonge.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ameitaka TRC kuhakikisha kuwa inashirikiana bega kwa bega na wathamini Ardhi wa Wilaya ya Maswa kuhakikisha wanajua thamani halisi ya ardhi ili wananchi watakaotwaliwa ardhi zao waweze kufaidika na fidia watakazo lipwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Bwana Simon Berege amelitaka Shirika la Reli Tanzania kuhakikisha zoezi la uhamishaji makaburi linafanyika kwa weledi na kufuata sheria na kanuni za maziko kwa kuhakikisha miili inazikwa kwenye maeneo yaliyotengwa na serikali ya Kijiji husika au Halmashauri na sio majumbani kama dhana za hapo awali .

Bwana Rashidi Mugo, Mwenyekiti Kijiji cha Muhida amewataka wananchi wa kijiji hicho kutambua umuhimu mradi wa SGR na kutokubali kudanganywa kuwa hawatalipwa stahiki zao kwani serikali inafuata sheria na kanuni na inatambua umuhimu wa wananchi na maendeleo yao.

“Wananchi wenzangu tuyakubali maagizo ya Serikali kwani mimi kama Mwalimu Mstaafu najua taratibu za Serikali na ulipaji fidia una taratibu zake na kwa kuwa nchi ni yetu sote tuyakubali mabadiliko, majukumu tumewapa viongozi tuwaache wafanye kazi tuliyowatuma” alisema Mzee Samwel Bugado kutoka Kijiji cha Muhida.

Tanzania Census 2022