Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MAENEO YAENDELEA KUTWALIWA MKOA WA PWANI KUPISHA MRADI WA SGR


news title here
06
April
2023

Shirika la Reli Tanzania – TRC linaendelea la zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi waliotwaliwa ardhi zao kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa – SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam – Morogoro katika mtaa wa Kwala, Makutupora pamoja na Kikongo wilayani Kibaha mkoa wa Pwani hivi karibuni Aprili, 2023.

Afisa Ardhi kutoka TRC Bi. Beatrice Luhimbo alisema kuwa zoezi lililofanyika ni kutokana na maeneo yaliyoongezwa na mkandarasi kwaajili ya ujenzi wa njia ya juu ya reli ya kisasa pamoja na eneo la kuweka udongo usiohitajika katika ujenzi.

“Mkandarasi anaongeza eneo pale anapokuwa na uhitaji kwasababu SGR ni mradi wa kusanifu na kujenga, ikitokea hivyo mwananchi anafanyiwa uthamini wa eneo na baadae anapatiwa stahiki zake” alisema Bi. Beatrice.

Mtendaji kutoka katika Kata ya Kwala iliyopo wilaya ya Kibaha Bw. Burton Mwaselela ameeleza kuwa wananchi wasisite kuendelea kutoa maeneo pindi yatakapohitajika ili kupisha ujenzi huo wa reli yenye kiwango cha kimataifa kwani reli hiyo italeta tija na chachu ya maendeleo kwatika maeneo itakapopita.

“Serikali inaweka juhudi kubwa kuhakikisha wananchi wanafaidi matunda ya kodi zao kupitia miradi mikubwa ukiwemo mradi huu wa SGR hivyo tuendelee kushirikiana na viongozi waliopo madarakani ili kuwapa nguvu ya kuinua taifa letu” alisema Bw. Mwaselela.

Mwananchi kutoka kijiji cha Makutupora Bw. Saidi Garama alisema kuwa mradi wa SGR utaleta mwangaza katika kukuza pato la taifa pamoja na wananchi, pia kwa kizazi cha baadae kwakuwa ni reli ambayo ina uwezo wa kudumu kwa miaka mingi.

Shirika la Reli Tanzania linaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha wanapata stahiki zao kwa kufuata utaratibu mzuri uliowekwa na Serikali na kusaidia kutatua changamoto yoyote inayojitokeza kwa wananchi waliotwaliwa maeneo yao.