Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MAENEO YAENDELEA KUTWALIWA MANYONI MKOANI SINGIDA


news title here
04
June
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliotwaliwa maeneo kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha tatu Makutupora - Tabora linalofanyika kwenye maeneo mbalimbali katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida hivi karibuni June, 2023.

TRC inaendelea na mchakato huo wa utwaaji ardhi ili kuhakikisha maeneo yote yanayohitajika na mkandarasi katika ujenzi yanakabidhiwa kwa wakati na kwa kufanya hivyo wananchi waliokwisha patiwa fidia wanapatiwa siku kadhaa ili kupisha ujenzi wa SGR.

Maeneo hayo yaliyotwaliwa ni pamoja na kijiji cha Kazikazi, Shuleni Mashariki, Galelaa , Genge 48 , Utemini, Upendo, Mlowa, Kitaraka, Mlongoji, Maendeleo, Mkola B, Kitopeni, Mrijeu, Msumbiji, Agondi, Mabondeni na Mapinduzi.

Afisa Ardhi kutoka TRC Bw. Ahsante Shadrack amesisitiza wananchi wote ambao wameshapatiwa malipo yao wazingatie muda waliopewa kwenye karatasi ya notisi inayowataka kuachia eneo ndani ya siku kumi na nne.

“Notisi inamtaka mwananchi ahame au aachie eneo baada ya siku kumi na nne ili mkandarasi asisimamishe ujenzi hivyo wanatakiwa kufuata maelekezo punde watakapo kabidhiwa malipo yao” alisema Bw. Ahsante.

Naye Mtendaji kutoka katika kijiji cha Kazikazi kilichopo Halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni Bw. Samwel Misanga alisema kuwa maeneo ambayo wananchi wametwaliwa ni pamoja na nyumba, mashamba, viwanja ambavyo wameridhia kwaajili ya kupisha ujenzi utakaoleta maendeleo katika vijiji vyao pamoja na kurahisha usafiri katika maeneo mbalimbali.

“Huu ujenzi ni mkubwa sana na manufaa tunaanza kuyaona kupitia sisi wenyewe maisha ya wanakijiji yanaanza kubadilika” alisema Bw. Misanga.

Timu kutoka TRC inashirikiana vyema na viongozi wa kijiji pamoja na wananchi kwa kuhakikisha kila aliyetwaliwa ardhi anapatiwa stahiki yake kwa kuambatanisha nyaraka ambazo zitamtambulisha kuwa anastahili kukabidhiwa malipo hayo ya hundi.