Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​MABEHEWA SITA YA GHOROFA YA TRENI YA KISASA YAPOKELEWA


news title here
09
June
2023

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Atupele Mwakibete apokea mabehewa sita (6) ya ghorofa yatakayotumika katika uendeshaji wa treni ya kisasa ya reli ya kiwango cha kimataifa - SGR, kwenye hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya bandari jijini Dar es Salaam Juni 9, 2023.

Mabehewa yaliyopokelewa ni sita (6) kati ya mabehewa thelathini (30) ya abiria yaliyonunuliwa na kufanyiwa maboresho na Kampuni ya Lueckemeier Transport and Logistic (GMBH) ya nchini Ujerumani.

Mhe. Mwakibete amesema kuwa Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania ina matarajio makubwa ya kukamilisha ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kwa haraka na ufanisi mkubwa ili kuweza kutoa huduma za usafiri wa reli kwa makusudio ya kukuza uchumi wa nchi na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

“Serikali ya awamu ya sita ilishaanza mchakato wa ununuzi wa mabehewa ya abiria na mizigo tumeshapokea mabehewa mapya 14 kati ya 59 kutoka nchini Korea Kusini na leo tunapokea mabehewa sita ya ghorofa kwaajili ya kuanza majaribio katika kipande cha kwanza cha mradi wa SGR pindi kichwa kimoja cha treni kitapowasili mwezi Julai mwaka huu” alisema Mhe. Mwakibete.

Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa amesema mabehewa sita ya ghorofayaliyopokelewa manne ni ya daraja la pili yenye uwezo wa kubeba abiria mia ishirini na tatu (123) na mabehewa mawili ni ya daraja la tatu yenye uwezo wa kubeba abiria mia na arobaini (140).

“Behewa moja lina uwezo wa mabasi matatu na lina mwendokasi wa kilomita mia sitini (160) kwa saa, ndani ya mabehewa kuna kiyoyozi, Runinga na CCTV kwaajili ya usalama wa abiria na mizigo” alisisitiza Ndugu Kadogosa

Naye Msemaji wa Serikali Ndugu Gerson Msigwa amesema mabehewa haya ya ghorofa ni ya historia kwa Tanzania, tangu nchi ipate uhuru ndiyo mara ya kwanza tunapokea mabehewa ya ghorofa.

“Hongera TRC Pamoja na maneno ya watu wachache mwenyenia ya kutuharibia lakini kazi inaendelea” alisema Ndugu Msigwa

Mhe. Edward Mpogolo Mkuu wa Wilaya ya Ilala alipotoa salamu za Mkoa wa Dar es Salaam kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema Treni ya SGR itaanza safari zake Dar es Salaam jiji la biashara lenye wakaazi zaidi ya milioni tano itakuwa ni chachu ya kukuza uchumi.

”Sisi ni mashuhuda wa ujenzi wa reli ya viwango vya kimataifa inayojengwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pongezi kwa TRC kwa kazi nzuri, na Uongozi wa Mkoa utaendelea kutoa ushirikiano kwenye ujezi wa mradi wa SGR” alisema Mhe. Mpogolo

Wizara ya ujenzi na uchukuzi kupitia Shirika la Reli Tanzania linaendelea kusimamaia ununuzi wa mabehewa ya abiria, vichwa vya treni, mabehewa ya mizigo 1430 na mitambo ya ukarabati wa njia ya reli ya SGR ili kuhakikisha inaboresha usafiri na usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli ya kisasa.

Mhe. Mwakibete amesisitiza nia ya Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha inaunganisha Bahari na Maziwa yote hapa nchini kwa njia ya SGR.