Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

MAADHIMISHO YA WIKI YA USALAMA WA RELI YAFUNGULIWA RASMI -TABORA.


news title here
09
October
2023

Mkuu wa Wilaya ya Uyui Bwana Zacharia Mwansansu afungua maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa reli katika uwanja wa Chuo cha Teknolojia ya Reli Tabora - TIRTEC Oktoba 09, 2023.

Maadhimisho ya wiki ya usalama wa reli mwaka 2023 yamebeba Kaulimbiu isemayo "Usalama Unaanza na wewe, Chukua Tahadhari" yanafanyika kwa ikishirikisha taasisi na mashirika mbalimbali ikiwemo Wizara ya Uchukuzi, LATRA, TRC, TAZARA , Chuo cha Usafirishaji Tanzania (NIT), Jeshi la polisi kikosi cha zima Moto na Uokoaji na mashirika mengine.

Mheshimiwa Mwansansu ambae ni mgeni rasmi amesema kuwa Serikali kupitia mashirika ya Reli Tanzania imekuwa ikitambua vyema umuhimu wa usalama na ulinzi wa miundombinu ya reli na wananchi kwa ujumla hivyo imeendelea kujenga miundombinu mipya na kuboresha iliyopo.

"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua vyema umuhimu wa ulinzi na usalama wa miundombinu ya reli na kwa ajili hiyo Serikali imeendelea kujenga na kuboresha miundombinu mipya ya reli ili uendeshaji uwe na tija na kuleta usalama" Amesema Mwansansu.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ameongeza kuwa usalama wa reli ni jukumu la watu wote hivyo linahitaji Ushirikiano wa pamoja kutoka idara za Serikali, Taasisi za umma, sekta binafsi, wadau na wananchi kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya udhibiti wa usafiri ardhini (LATRA) Bwana Habibu Suluo ameeleza kuwa wananchama wa Shirikisho la Mashirika ya Reli kwa nchi zilizomo kusini mwa Afrika ( SARA) wamekuwa wakishirikiana katika kuunda kanuni na kutunga Sheria mbalimbali zinazodhibiti usalama na kuhakikisha Usalama wa Reli unaheshimika.

"Wanachama wa moja kwa moja wa SARA yani LATRA, TRC na TAZARA tumekuwa tukishirikiana na wenzetu ambao wameanza mapema haswa kwenye kutunga Sheria za reli ili kuhakikisha Usalama unaheshimika" Amesema Suluo.

Bwana Suluo amewasihi wananchi kuchukua tahadhari wanapopita kwenye makutano ya Reli na Barabara na kuzingatia alama za usalama ili kuimarisha usalama na kuepusha ajali za mara kwa mara .

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu kutoka Shirika la Reli Tanzania ambae ni Mkuu wa Chuo cha Teknolojia ya Reli Tabora (TIRTEC) Bwana Damas Mwajanga amesema kuwa Shirika la Reli Tanzania linaendelea kuimarisha usalama wa reli kwa kukarabati njia za reli, mabehewa, vichwa vya treni na kuongeza uelewa kwa wananchi.

"Shirika la Reli tumeendelea kuzingatia kanuni na miongozo ya kiusalama, kampeni za uelewa zimekuwa zikifanywa haswa katika miradi yetu ya SGR kuhusu usalama na ulinzi, ukarabati mkubwa wa mabehewa umefanywa na pia watumishi wa reli wanapelekwa kwenye mafunzo mbalimbali yanayo husu usalama" Amesema Bw. Mwajanga.

Shughuli za maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli zinaendelea ikiwemo maonesho ya huduma zitolewazo na mashirika ya Reli , kampeni za uelewa kuhusu usalama wa reli kwenye mashule, mitaa na maeneo mbalimbali ya mji wa Tabora kuelekea kilele cha maadhimisho hayo Oktoba 13, 2023 katika viwanja vya chuo cha TIRTEC.

Wananchi wanakumbushwa kuwa usalama ni muhimu katika usafiri wa reli hiyvo Shirika la Reli Tanzania linawasihi wazingatie matumizi ya alama kwenye maeneo ya vivuko, hifadhi ya reli na maeneo ya miradi.