Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​KONGO YAVUTIWA NA MAENDELEO YA MRADI WA SGR NCHINI


news title here
24
October
2022

Shirika la Reli Tanzania – TRC limepokea ugeni wa Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Felix Tshilombo Tshisekedi kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro katika stesheni kuu ya SGR jijini Dar es Salaam Oktoba 24, 2022.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makamu Mbarawa amesema kuwa ziara ya Mhe. Tshisekedi ina lengo la kuona maendeleo ya mradi wa ujenzi wa SGR kufuatia nia ya serikali tatu ikiwemo Tanzania, Kongo na Burundi ya kuunganisha reli ya kisasa kutoka bandari ya Dar es Salaam mpaka Kindu nchini Kongo.

”Kwa mara mbili tumekutana na Waziri wa ujenzi wa Kongo na kuweka makubaliano maalumu kwaajili ya ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Uvinza, Kitega mpaka Kindu (DRC) ambapo nimeshirikiana na Waziri wa ujenzi wa Kongo pamoja na Burundi” alisema Prof. Mbalawa.

Prof. Mbalawa alieleza kuwa mchakato wa kufungua tenda ya kazi katika kipande cha kutoka Uvinza mpaka Kitega nchini Burundi upo mbioni kukamilika ili kupata mkandarasi wa kipande hicho ambapo kipande kinachofuata cha kutoka Kitega, Burundi mpaka Kindu wataalamu wanaendelea kufanya tafiti ya kujua gharama itakayotumika.

“Umuhimu wa ujenzi huu utakaotoka Uvinza mpaka DRC ni mkubwa kwa kurahisisha ubebaji wa mizigo kupitia treni ambapo itapunguza gharama na muda wa safari” aliongezea Prof. Mbarawa.

Mwenyekiti wa Bodi TRC Prof. John Kondoro alisema kuwa ujio wa mara ya pili wa Mhe. Raisi wa Kongo unaendelea kumpa hamasa ya alichokiona kupitia mradi wa ujenzi wa SGR kwaajili ya kuunganisha reli kutoka Uvinza hadi Kongo.

“Hiki ambacho kimejengwa hapa ndio reli itakayojengwa sehemu yote yenye kiwango cha SGR kutoka hapa (Dar es Salaam), Tabora, Kigoma, Uvinza, Msongati, Kitega hadi Kongo” alisema Prof. Kondoro.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ameeleza kuwa wathamini wameanza kufanya kazi kutoka Kitega kwenda Kindu kupitia mpango unaondelea wa ujenzi wa reli kutoka Uvinza, Kitega, Burundi, Uvira mpaka Kindu.

”Tunategemea mpaka mwezi wa pili uendeshaji wa treni ya kisasa utaanza rasmi, japo uendeshaji wa ndani unaendelea kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma” alisema Ndugu Kadogosa.

Aidha, Ndugu Kadogosa alisema kuwa Kipande cha kwanza kimefikia asilimia 97.47, kipande cha pili kimefikia asilimia 90.01. kipande cha tatu kimefikia asilimia 01.94, kipande cha nne kipo kwenye mchakato wa ufunguzi na kipande cha tano kimefikia asilimia 14.49.

Mradi wa ujenzi wa SGR utakua chachu ya maendeleo katika nchi za Jirani mwa Tanzania pamoja na Afrika kwa kusafirisha bidhaa na mizigo mbalimbali pamoja na kuinua biashara ndogondogo kwa wafanyabiashara na wasafiri kupitia reli hiyo ya kisasa.