Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

KISHINDO CHA SGR KUFUNGUA MILANGO YA DHAHABU KIGOMA


news title here
21
July
2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Tabora hadi Kigoma chenye urefu wa kilomita 506.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amesisitiza kuwa mradi huo wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 2.74 (takribani shilingi trilioni 7.4) utakuwa mkombozi mkubwa wa kiuchumi kwa wananchi na ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati.

"Kigoma haitakuwa tena mwisho wa reli kama ilivyokuwa ikifahamika, bali itakuwa mwanzo wa kufunguka kwa fursa za biashara, ajira na uwekezaji. Mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam sasa itafika moja kwa moja Kigoma kwa haraka na uhakika," alisema Mhe. Dkt. Samia.

Aidha, mradi huo unatarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, uvuvi na ujasiriamali. Wakulima watapata pembejeo kwa gharama nafuu na masoko mapana ya mazao yao, huku wafanyabiashara na vijana wakipata fursa mpya za ajira kupitia mtandao wa usafirishaji, maghala na huduma za kiuchumi zitakazostawi.

Zaidi ya hayo, kuimarishwa kwa miundombinu hiyo kutaiweka Kigoma kuwa kitovu cha kimkakati kinachounganisha Tanzania na nchi jirani za Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo na Zambia. Hatua hii itarahisisha mnyororo wa biashara na usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa Maziwa Makuu.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amebainisha kuwa mradi huo wa SGR ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kujenga mfumo jumuishi wa usafirishaji, huku akiahidi kusimamia utekelezaji wake kwa weledi na viwango vya juu ili ukamilike kwa wakati.