Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

KILELE CHA MAADHIMISHO YA WIKI YA USALAMA TABORA


news title here
13
October
2023

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Dkt. Ally Possi afunga maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli katika uwanja wa chuo cha Teknolojia ya Reli Tabora - TIRTEC Oktoba 13, 2023.

Maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli Tanzania mwaka 2023 yamebeba Kauli mbiu isemayo "Usalama Unaanza na Wewe, Chukua Tahadhari" umefikia kilele baada ya kampeni ya uelewa iliyofanywa na TRC kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini - LATRA, TAZARA na Chuo cha Usafirishaji - NIT.

Kampeni ya uelewa na uhamasishaji imefanywa katika shule, masoko, vituo vya mabasi, vituo vya madereva wa bodaboda, sehemu zenye mikusanyiko ya watu pamoja na maonesho ya bidhaa na huduma zitolewazo na taasisi husika ili kujenga hamasa, uelewa na kutoa elimu kuhusu masuala ya ulinzi na Usalama wa reli.

Dkt. Ally Possi amesema kuwa Kauli mbiu ya mwaka 2023 katika maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli imebeba ujumbe unaogusa maisha ya watu hivyo kuwataka wananchi wazingatie swala la Usalama na kujilinda bila kushurutishwa kutoka Mamlaka za Serikali.

"Ukitafakari Kauli mbiu hii," Usalama Unaanza na Wewe, Chukua Tahadhari" utaona umebeba ujumbe mkubwa Sana katika maisha yetu ya kila siku, kila kitu tunachokifanya tunapaswa kufikiria Usalama ili tuchukue hatua madhubuti" amesema Dkt. Possi.

Aidha, Possi ameongeza kuwa serikali kupitia Shirika la Reli la Tanzania imejikita katika kujenga miundombinu mipya na kuboresha miundombinu iliyopo ili kuhakikisha usafiri wa Reli unakuwa salama kwa usafirishaji wa abiria na mizigo na kuwezesha nchi kukua kiuchumi.

"Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kujenga mtandao wa reli nchi nzima na hivi punde tutaanza ujenzi wa kipande cha Tabora - Kigoma hizi zote nikuwezesha nchi yetu kukua kiuchumi kwa kujenga miundombinu ya kisasa na yenye ulinzi na Usalama zaidi" amesema Dkt. Possi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya LATRA Profesa Mohammed Ahmed Amme amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa chuo cha Teknolojia ya Reli Tabora - TIRTEC katika kutoa elimu inayolenga kuleta mapinduzi katika sekta ya Reli LATRA imeazimia kushirikiana na Chuo ili kuongeza ufanisi na kufikia malengo.

"Kwa kutambua umuhimu wa TIRTEC katika kutoa elimu inayolenga kuleta mapinduzi kwenye masuala ya Teknolojia ya Reli ikiwa ujenzi wa behewa ,kufanya utafiti mbalimbali na kutoa mafunzo ya uendeshaji wa Reli, LATRA itajidhatiti katika kushirikiana na Chuo hiki ili kuongeza ufanisi" amesema Profesa Amme.

Mkuu wa Chuo cha Teknolojia ya Reli Tabora - TIRTEC Bwana Damas Mwajanga ameeleza kuwa Shirika la Reli Tanzania limeendelea kutekeleza mkakati wa kupunguza na kudhibiti ajali katika mtandao wa reli ambapo kupitia chuo cha TIRTEC kimeandaa mtaala mahususi unaohusu Usalama wa Reli.

"Katika kuandaa wananchi kupokea mradi kampeni za usalama zimeendelea kufanyika na kutambua hivo, TRC kupitia Chuo cha Reli Tabora kimeandaa mtaala maalumu unaohusu Usalama wa Reli, mtaala huu utazalisha wataalamu watakao ongeza ufanisi na Usalama wa shughuli za Reli" amesema Bwana Mwajanga.

Wananchi wanaendelea kuhamasishwa kutofanya shughuli za kijamii kwenye reli au pembezoni mwa reli ili kuondoa na kupunguza ajali zinazo weza kuzuilika.