KIHENZILE AITAKA TRC KUIMARISHA MIFUMO YA KIDIGITI KUTOA HUDUMA

June
2025
Wizara ya Uchukuzi imelitaka shirika la Reli Tanzania (TRC) kuendelea kutoa huduma bora kupitia mifumo ya kidigiti ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji ya abiria.
Hayo yamesemwa Juni 19, 2025 na Naibu Waziri Wizara ya Uchukuzi Mhe. David Kihenzile, alipolitembelea banda la maonesho la TRC katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanoendelea Jijini Dodoma.
Mhe. Kihenzile amesema kuwa TRC kupitia mifumo ya ukataji tiketi mtandaoni uendelee kuboreshwa ili kukidhi mahitaji ya abiria na kuondoa usumbufu pindi abiria anapotaka kusafiri.
"TRC mnafanya vizuri sana muendelee kufanya kazi kwa utumishi uliotukuka ila niwaombee mboreshe mfumo wa ukataji tiketi, uwe rafiki kwa abiria pindi anapotaka kubadilisha safari au kubadilisha daraja alilokata, tunataka abiria wote wafurahie kusafiri na treni zetu, ili ni jambo dogo lifanyiwe kazi" Amesema Mhe. Kihenzile.
Aidha, Mhe. Kihenzile amewapongeza wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania kwa kusimamia ujenzi wa mradi wa SGR na kuendelea kutoa huduma za usafiri wa treni zote mbili MGR na SGR kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu.
" Wafanyakazi wa TRC nawapongeza saana, mmeweza kusimami vyema ujenzi wa SGR mpaka hapa tulipofikia na mnaendelea kutoa huduma bora sana, muendelee hivyo hivyo ili kuipaisha Tanzania ndani na nje ya nchi" Amesema Naibu Waziri Mhe.Kihenzile.
Shirika la Reli Tanzania linaendelea kutoa huduma za usafiri wa reli za MGR na SGR ili kukidhi mahitaji ya Watanzania wote wa miji na vijiji na wavipato vyote na kuendelea kukuza uchumi wa nchi. Maadhimisho ya Wiki ya Umma yaliyoanza Juni 16, 2025 yanatarajiwa kufikia tamati yake Juni 23, 2025.