Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​KATIBU MKUU KIONGOZI ATEMBELEA MRADI WA UJENZI WA RELI YA KISASA DAR – MORO


news title here
21
December
2021

Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Hussein Kattanga atembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha Dar es Salaam – Morogoro ikiwa ni ziara ya kikazi kuona maendeleo ya mradi wa SGR, Disemba 20, 2021.

Katika ziara hiyo Mhe. Balozi Katanga aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Bw. Gabriel Migire, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Kondoro pamoja na menejimenti ya Shirika la Reli.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Bw. Gabriel Migire ameeleza kuwa lengo la ziara ni kumfahamisha Katibu Mkuu kiongozi na kumpitisha katika reli ya kisasa ambayo inajengwa kwakuwa yeye ni mtendaji mkuu wa Serikali pamoja na kwamba alikuwa anapata taarifa lakini kuona ni kuamini.

Katibu mkuu aliongeza kuwa “Katibu Mkuu Kiongozi ameridhishwa na kazi kubwa iliyofanyika, ameona kwa mara ya kwanza nchi imefanya uwekezaji mkubwa na ametutaka tuhakikishe tunafikia matarajio ya nchi na tunaweka mazingira mazuri ya kutafuta bidhaa na masoko katika reli hii ya kisasa”

“Tumetokea Pugu hadi Morogoro kwa treni, tumeshafanya manunuzi ya vichwa na behewa kwa ajili ya kuanza majaribio, lakini watengenezaji wana changamoto ya UVIKO19 kwahiyo tulishindwa kupata vichwa na behewa, tulitarajia kufanya majaribio mwezi Disemba lakini kutokana na changamoto ya UVIKO19 vichwa na behewa vitapokelewa kuanzia mwezi Machi 2022” aliongeza Katibu Mkuu

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya akurugenzi Prof. John Kondoro amesema kuwa ni mara ya kwanza Katibu Mkuu Kiongozi kutembelea mradi wa SGR na ilikuwa fursa kwa Shirika kuelezea mafanikio, changamoto pamoja na mipango ya Shirika ikiwemo uendelezaji wa mradi wa SGR kutoka Mtwara hadi Bamba Bay, Tanga hadi Musoma, Dar es Salaam hadi Mwanza, Kigoma na nchi za jirani.

Aidha, Prof. Kondoro alieleza kuwa Katibu Mkuu alipata ufafanuzi kuhusu mafanikio ya Shirika katika utoaji huduma na namna ambavyo Shirika linashirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania – TPA katika kuhakikisha huduma ya usafirishaji shehena inaimarika nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa amesema kuwa Katibu Mkuu Kiongozi alipata taarifa ya Shirika hususani katika mradi wa ujenzi wa reli kisasa ambapo Katibu Mkuu ameridhishwa na kazi na ametoa maagizo kwa uongozi wa Shirika kwa ajili ya kuboresha utendaji.