Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​KATIBU MKUU CCM: SGR MWAROBAINI WA ADHA YA MTO MKONDOA


news title here
31
January
2023

Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo ametembelea Stesheni ya Reli ya kisasa, Kilosa mkoani Morogoro iliyopo katika kipande cha pili cha mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa SGR, Morogoro – Makutupora, Januari 30, 2023.

Stesheni ya SGR Kilosa ni moja kati ya vituo vya ziara ya Katibu mkuu Chongolo wilayani Kilosa, yenye lengo la kuwatembelea wananchi na kusikiliza changamoto zao ili kuzitafutia ufumbuzi.

Akiwa stesheni ya SGR Kilosa, Ndg. Chongolo ameeleza kuwa ujenzi wa reli ya kisasa umeleta ufumbuzi wa kero ya muda mrefu ya miundombinu ya reli kusombwa na maji kipindi cha mvua.

“Kilosa lilikuwa ni eneo ambalo reli ya kati inapata madhara makubwa mvua ikinyesha, kutokana na mto Mkondoa palikuwa pana athirika sana kuliko mahali popote, lakini sasa ni tofauti kutokana na miundombinu hii ya kisasa”

Stesheni ya SGR ya Kilosa ni moja kati ya vituo vya kati vya Reli hiyo, ambacho kinategemewa kuhudumia wananchi wa wilaya ya kilosa na maeneo jirani ukiwemo mkoa wa Iringa na kupitisha watalii kuelekea Hifadhi ya Taifa ya mikumi.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Reli ya kisasa Mkurugenzi mkuu wa TRC Masanja Kadogosa, amesema kuwa hadi sasa ujenzi wa reli hiyo unaendelea vizuri ambapo kipande cha Dar es salaam – Morogoro kimefikia zaidi ya 97%, kipande cha Morogoro – Makutupora zaidi ya 91%, Makutupora – Tabora 3.95%, Tabora – Isaka 1% na kipande cha Mwanza – Isaka zaidi ya 22.7%.

Aidha mkurugenzi mkuu Kadogosa amesema kuwa ujenzi wa reli ya kisasa utakapokamilika utakuwa na manufaa makubwa katika sekta ya Biashara na uwekezaji, ambapo katika kipindi cha ujenzi, awamu mbili za ujenzi wa SGR zitatengeneza zaidi ya ajira 40,000 huku thamani ya dhabuni zilizotolewa kwa wakandarasi wa ndani zikifikia zaidi ya shilingi Trilioni 1.8.

Aidha katibu mkuu Chongolo ameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa lengo la kuwaletea maendeleo watanzania.

“nimpongeze Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka kipaumbele katika kuhakikisha ujenzi wa Reli hii unafanyika kwa kasi lakini kwa vipande vingi vinavyounganisha Dar es salaam hadi Mwanza na Dar es Salaam hadi Kigoma”

Pamoja na mambo mengine Katibu mkuu Chongolo amesisitiza juu ya umuhimu wa kulinda miundombinu ya reli kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

Pamoja na wananchi wa wilaya ya Kilosa, Mbunge wa Kilosa Prof. Paramagamba Kabudi, Mbunge wa Mikumi Denis London a Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka walihudhuria ziara hiyo.