KASI YA UJENZI SGR YAENDA SAMBAMBA NA UTWAAJI ARDHI

June
2023
Shirika la Reli Tanzania – TRC linaendelea na shughuli za ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa – SGR awamu ya kwanza na ya pili sambamba na utwaaji ardh katika maeneo mbalimbali nchini ili kupisha mradi ikiwemo mkoani Singida na Tabora, Juni 2023.
Lengo la utwaaji ardhi ni kukabidhi maeneo kwa mkandarasi wa mradi wa SGR kipande cha tatu Makutupora – Tabora ili aweze kuendelea na ujenzi wa mradi na kukamilisha kwa muda uliopangwa. Zoezi linaendelea mkoani Singida na Tabora ambapo zaidi ya wananchi 200 waliotwaliwa maeneo yao na baadaye kufanyiwa uthamini wanalipwa fidia ili kupisha mradi.
Maeneo ambayo wananchi wamelipwa fidia katika wilaya za Tabora, Uyui, Sikonge, Manyoni na Itigi ni pamoja na Makutupora, Saranda, mabondeni, Tambuka Reli, Kipondola, Aghondi, Kitopeni, Kazikazi, Tura, Karangasi, Nyahua, Kamama, Igalula, Itulu, Milembela na Chang’ombe.
Maeneo yaliyotwaliwa ni kwaajili ya kuchimba kifusi, kutupa kifusi na maeneo ya kuzalisha kokoto. Wananchi waliotwaliwa maeneo wamelishukuru Shirika kwa kuharakisha kulipa stahiki zao na wameonesha imani kubwa kwa Serikali kuwa miradi ya kimkakati inakwenda kuleta maendeleo hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kutoa ushirikiano.
“Shirika la Reli kupitia mradi wa SGR wameweza kutwaa sehemu ya eneo langu kwaajili ya kuchimba kifusi lakini nachopenda kushukuru ni kwamba wamejitahidi kufanya kila liwezekanalo kulipa fidia. Kwahiyo leo nashukuru wamenipa hundi yangu, naomba wananchi wote kwa maeneo haya ambayo yanatwaliwa watoe ushirikiano mradi uweze kupita na maendeleo yapatikane” alisema bwana Anselim Tendwa, Mkazi wa Itulu, Tabora.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyahua Bwana Abdallah Katoto amesema kuwa “Serikali inajitahidi kuboresha maisha ya wananchi wake, nashukuru leo imekuja kulipa fidia ili kupisha mradi huu wenye manufaa, hapa (Nyahua) kutakuwa na Stesheni ni suala ambalo wananchi wa wilaya ya Sikonge walikuwa wanalitaka, hivyo wanaishukuru Serikali kwasababu Stesheni hii itaunganisha Sikonge na mikoa ya jirani ikiwemo Mbeya na Katavi”.
Zoezi la ulipaji fidia ni endelevu katika maeneo ambayo mradi wa SGR umepita, linafanyika kwa kufuata taratibu na Sheria ikiwemo Sheria ya Uthamini na Sheria ya Fidia ambapo viongozi wa maeneo husika na wananchi wanahusishwa kuanzia mchakato wa kutambua maeneo, uthamini, utoaji taarifa hadi utoaji fidia.