Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​KASEKENYA ATEMBELEA BANDA LA TRC SABASABA


news title here
06
July
2023

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Godfrey Kasekenya atembelea banda la Shirika la Reli Tanzania - TRC lililopo katika maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya kilwa jijini Dar es Salaam Julai, 2023.

Mhe. Kasekenya alisema kuwa banda la TRC limepangika vizuri kwa kuona vifaa vyenye historia ya reli vilivyokuwa vikitumika miongo iliyopita hadi kufikia mageuzi makubwa ya teknolojia ya miundombinu ya reli yanayofanyika kwenye ujenzi wa reli ya kisasa - SGR.

Mhe. Kasekenya ameeleza kuwa mageuzi ya ujenzi wa reli ya kisasa - SGR yatakua kichocheo cha uchumi wa taifa la Tanzania kwakua upanuzi wa bandari unatakiwa kwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji hususani reli ambayo ndiyo njia kuu ya usafirishaji wa mizigo mizito kwa nchi za jirani ambazo hazina bandari.

"Nawaasa wananchi wajitokeze kwa wingi kwenye banda la TRC wapate kuona fursa mbalimbali zilizopo kwenye ujenzi wa mradi wa SGR" alisema Mhe. Kasekenya.

Mhe. Kasekenya amewashauri wananchi kutumia fursa hiyo ya kutembelea maonesho ya Sabasaba ili kukutana na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kukuza mtandao wa biashara.

"Wale wanaojichukulia taarifa kwenye vyanzo ambavyo si rasmi huu ni wakati muafaka kuja kuonana na watu sahihi ili kupata taarifa sahihi" alisisitiza Mhe. Kasekenya

Maonesho ya 47 ya biashara ya kimataifa yenye kaulimbiu isemayo "Tanzania mahali sahihi kwa biashara na uwekezaji" yamefunguliwa rasmi tatehe 5 Julai 2023 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa na yanatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 13 Julai 2023.