KAMPENI YA UELEWA KWA JAMII KUHUSU MRADI WA UJENZI WA SGR, MWANZA – ISAKA YAPIGA HODI KWIMBA MKOANI MWANZA

July
2021
Shirika la Reli Tanzania – TRC linaendelea na kampeni maalum ya kutoa elimu ya uelewa kuhusu Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR, kipande cha tano, Mwanza – Isaka (Km 341), kwa jamii zinazoishi maeneo ya kanda ya ziwa.
Kufuatia kampeni hiyo timu ya mawasiliano kutoka Shirika la Reli Tanzania TRC, imetembelea ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza ikiwa ni sehemu ya hatua muhimu ya Utekelezaji wa mradi kwa kuhakikisha uelewa Sahihi kwa viongozi na Wananchi juu ya masuala yanayohusu mradi ili kuifikia shabaha ya maendeleo ya Mtanzania mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kupitia uimarishwaji wa sekta ya miundombinu ya Reli nchini.
Aidha wataalam hao kutoka vitengo mbalimbali vya Shirika la Reli Tanzania, walipata nafasi ya kuwasilisha ujumbe wa Kampeni hii katika kikao cha maandalizi ya Mapokezi ya mbio za Mwenge Wilayani Kwimba, kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya ya Kwimba Mhe.Johari Samizi na kuhudhuriwa na Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, viongozi wa ngazi ya Wilaya na Kata pamoja na Taasisi binafsi.
Akiwatambulisha wataalamu hao katika kikao hicho, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano TRC Bi. Jamila Mbarouk, ameeeleza kuwa lengo hasa la kufika katika kikao hicho, ni kufikisha ujumbe wa kampeni ya Uelewa Kuhusu mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa, na Kuhakikisha viongozi wanakuwa na Uelewa sahihi wa masuala yanayohusu mradi ili kurahisisha elimu kuwafikia Wananchi na hatimaye kurahisisha hatua zinazofuata katika Utekelezaji wa mradi, ikiwemo zoezi la utwaaji ardhi.
Kwa upande wake meneja Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR kipande cha Mwanza hadi Isaka, Mhandisi Machibya Masanja ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huu wa kimkakati unaenda sambamba na faida mbalimbali ikiwemo fursa za ajira za moja kwa moja 11,000, akiongeza kuwa Zaidi ya watu 75,000 watanufaika na ajira zisizo za moja kwa moja.
Kwa upande mwingine, viongozi hao waliweza kupata nafasi ya kuuliza maswali juu ya masuala mbalimbali yanayohusu mradi ikiwemo fidia na Utwaaji ardhi, ambapo Afisa Mwandamizi kutoka Kitengo cha Ardhi TRC Bw. Fredrick Kusekwa ameeleza kuhusu taratibu na Sheria zinazoongoza zoezi la utwaaji ardhi sambamba na sifa za anayestahili kulipwa fidia.
Aidha Bw. Kusekwa ameeleza kuwa, katika utekelezaji wa mradi huu wenye thamani ya zaidi ya Sh. Trilioni 3. za Kitanzania, kila ambaye eneo lake litatwaliwa kwaajili ya ujenzi, atalipwa kulingana na anavyostahili.
Akizungumza baada ya ujumbe huo kutoka Shirika la Reli Tanzania, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Johari Samizi, amewashukuru wataalam hao kutoka TRC na kuahidi ushirikiano wa dhati kwa kipindi chote ambacho mikutano ya hadhara ya Kampeni hiyo itakuwa ikifanyika Wilayani Kwimba.
“Tunafahamu watakwenda kukutana na viongozi wa ngazi za chini na wananchi wa hapa Kwimba ambao ndio wamiliki wa hayo maeneo, lakini sisi kwa ngazi ya Wilaya tutahakikisha kunakuwa na ulinzi na usalama kwa timu hii, ili kazi ifanyike kama ilivyokusudiwa”
Mbali na Mikutano ya hadhara na Wanachi, ili kufikisha ujumbe kwa ufanisi Zaidi, kampeni hii ambayo ni endelevu vilevile inafanyika kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii, amabapo kwa hatua hii ya awali, mikutano ya hadhara inafanyika katika mikoa ya Mwanza, Simiyu na Shinyanga.