Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​KAMPENI YA UELEWA KUHUSU MRADI WA SGR KIPANDE CHA NNE TABORA –ISAKA YAANZA


news title here
26
March
2023

Shirika la Reli Tanzania limeanza utoaji wa elimu kwa wananchi wa mkoa wa Tabora kuhusu mradi wa SGR kipande cha nne Tabora –Isaka chenye jumla ya kilomita 165, Machi 2023.

Meneja msaidizi wa mradi wa SGR kipande cha nne Mhandisi Abduli Habib akiwa na watendaji wa kada mbalimbali kutoka TRC walifika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora na kuonana na Kaimu Afisa Tawala wa Mkoa wa Tabora Ndugu Daniel Barangu na kumueleza lengo la kufanya kampeni ya uelewa wa mradi wa SGR kipande cha nne Tabora - Isaka, ni kuwapatia elimu wananchi kuhusu mradi wa SGR na mambo mengine yatakayowagusa wananchi watakaopitiwa na mradi ikiwemo kutwaaliwa ardhi yao. Wananchi watajulishwa utaratibu utakaotumika kupima ardhi na ulipaji fidia kwa vyote ambavyo haviamishiki vitakavyokutwa kwenye ardhi .

Mhandisi Abdul Habib amemjulisha Kaimu Afisa Tawala Mkoa wa Tabora kuwa wananchi watapewa elimu kuhusu ulinzi na usalama wa reli, watajulishwa mambo ya kuzingatia ili kudumisha uhusiano mwema kati ya jamii na watekelezaji wa mradi, watapatiwa elimu kuhusu mazingira, utaratibu wa kupata ajira kwa mkandarasi, wataelekezwa utaratibu wa kuwasilisha maoni au malalamiko kuhusu mradi na mwisho watapewa nafasi ya kuuliza maswali na kupatiwa majibu.

Ndugu Baragu ameipongeza TRC kwa utoaji elimu mapema kuhusu mradi wa SGR kipande cha nne Tabora - Isaka kwa kusema wananchi wanayo maswali mengi ambayo yanahitaji ufafanuzi, kwa elimu hii kwenda kutolewa kabla ya mradi kuanza itapunguza malalamiko kwa kuwa wananchi watakuwa na uelewa kuhusu mradi na stahiki watakazolipwa kwa maeneo yatakayopitiwa na mradi.

“Mradi wa SGR kwa mkoa wa Tabora utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi, natoa wito wakazi wote wanaopitiwa na mradi kutoa ushirikiano kwa TRC na Mkandarasi ili kuhakikisha mradi huu haukwami” alisema Ndugu Barangu

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Luis Peter Bura amesema wanatarajia ajira zitakazotolewa na mkandarasi zitatoa kipaumbele kwa wananchi wenye sifa wanaopitiwa na mradi.

“Ni aibu kwa wakazi wa Tabora wanaopewa ajira na Mkandarasi na kugeuka wezi wa mali za Mkandarasi, sifa mama ya kuajiriwa iwe ni uaminifu” alisisitiza Mhe Bura.

Kampeni ya uelewa kuhusu mradi wa SGR kipande cha nne Tabora – Isaka itafanyika kwa zaidi ya wiki mbili katika Wilaya ya Tabora, Uyui na Nzega katika vijiji thelathini na moja (31).