Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​KAMATI ZA BUNGE ZASAFIRI KWA SGR DODOMA HADI DAR ES SALAAM


news title here
27
September
2022

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Kamati ya Uwekezaji Mitaji ya Umma zimefanya ziara ya kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR unaotekelezwa na Shirika la Reli Tanzania - TRC kuanzia Dodoma hadi Dar es Salaam kwa kutumia treni ya uhandisi ya SGR Septemba 26, 2022.

Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso amesema “leo tumefanya ziara kutembelea mradi wa SGR unaotekelezwa na TRC na kujionea namna mradi huo unavyotekelezwa”,

Mhe. Kakoso ametoa wito kwa Shirika la Reli na kuwataka washirikiane na Serikali kuhakikisha reli inafika katika nchi za jumuiya ya Afrika mashariki.

"Tunawaomba TRC kufanya jitihada kwa kushurikiana na Serikali kuhakikishaa kipande cha kutoka Tabora - Kigoma kinakamilika haraka. Lakini tunaiomba Serikali wafanye jitihada ya kuunganisha nchi jirani hasa Kongo ambako kuna mizigo mingj na yenye tija katika bandari zetu kwa hufanya hivyo tutaona faida kubwa ya uwekezaji katika reli yetu" alisema Mhe. Kakoso.

Vilevile Mhe. Kakoso amebainisha kuwa endapo mradi wa SGR utavuka mipaka kwenda nchi jirani kama Kongo, Sudani kusini na Burundi bandari za Dar es Salaam, Mwanza na Tanga zitanufaika na kuongeza uchumi wa nchi na kuchochea maendeleo kwa watanzania.

"Tunaamini endapo Serikali itawekeza katika kupeleka SGR kwenye nchi jirani tutapanda kutoka asilimia 37% za mizigo tunazopata kutoka bandari ya Dar es Salaam, tuna uwezo wa kufika 60% mpaka 70% kwasababu tutakua na eneo kubwa la upitishaji mizigo kutoka Kongo kupitia Zambia kupitia bandari ya Kalemi kuja bandari Karema na kuunganisha reli ya kutoka Mpanda hadi Dar es Salaam." aliongeza Mhe. Kakoso.

Pia, Mhe. Kakoso ameieleza TRC kuwa, kutakuwa na mzigo mwingine mkubwa kutoka Uganda kupitia bandari ya Dar es Salaam na Tanga ambapo kutakuwa na kiwango kikubwa cha ubebaji mizigo kutoka 2% ya mzigo inayopitia bandari ya Dar es Salaam na kufikia 30%, hivyo mizigo ya Uganda ikipitia bandari ya Dar es Salaam tutateka soko la Sudani Kusini.

Kwa upande wake George Malima, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji Mitaji ya Umma amesema lengo la ziara ni kuona kazi inayofanyika na kwenda kuwaambia wananchi kile ambacho wamekiona.

"Tumeona kwa macho yetu uwekezaji mkubwa uliofanyika na unaoendelea tunaipongeza TRC kwa usimamizi mzuri. Sisi kama wawakilishi wa wananchi tunakuwa katika nafasi nzuri ya kuwaambia wananchi uhalisia wa mradi" alisema Mhe. Malima.

Mhe.Malima aliongeza kuwa “mradi huu umejengwa katika ustadi mkubwa sana na tunaiona fedha iliyotumika, niwaombe TRC na watanzania kwa ujumla kuwa walinzi wa miundombinu hii, kwa kufanya hivyo tutakuwa na fursa ya kuwavutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini".

Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa akijibu swali la Mhe. Kakoso, ameelezea ni kwa namna gani Shirika limejipanga kulinda miundombinu dhidi ya uhujuma.

"Tunashirikiana na vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuhakikisha miundombinu hii inabaki salama, katika stesheni zote tumejenga vituo vya polisi ili kuhakikisha usalama wa miundombinu na abiria sambamba na hivyo Shirika linaendelea kutoa elimu ya uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa wananchi kuhusika katika ulinzi wa miundombinu ya reli" alisema Mkurugenzi Mkuu TRC.

Wajumbe waliridhishwa na maendeleo ya mradi kwani wamepata fursa ya kusafiri kwa reli ya SGR kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam umbali wa Km 444. Wajumbe ambao ni wawakilishi wa wananchi Bungeni wameileza TRC kuwa wataende kuwa mabalozi wazuri katika kuutangaza mradi na kuusemea kwa wananchi.