Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA THAMANI YA FEDHA KATIKA MRADI WA SGR


news title here
23
March
2023

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikiongozwa na Makamu mwenyekiti wa kamati Mhe. Japheth Hasunga imefanya ziara katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kuanzia Morogoro hadi Dar es Salaam Machi 20, 2023.

Lengo la ziara ni kukagua mradi na kutathmini matumizi ya fedha za umma zilizowekezwa katika mradi wa SGR kwa lengo la kuleta manufaa kwa wananchi katika nyanja zote za maendeleo. Kamati ya PAC ina dhima kubwa ya kushughulikia na kusimamia matumizi ya fedha za umma katika Wizara, Idara, Wakala na Mashirika ya Umma.

“Tumetembelea ujenzi wa miundombinu ya SGR na tumepanda treni kuanzia Morogoro hadi Dar es Salaam, tumejifunza mambo mengi na tumejionea uwekezaji mkubwa umefanywa na Serikali ya awamu ya tano na ya sita” alisema Mhe. Hasunga

Makamu Mwenyekiti amesisitiza kuwa “Kamati yangu imeshuhudia mabehewa mapya ya SGR ni mazuri na mapya tofauti ya yalivyokuwa yanaonekana kwenye mitandao, kamati imeweza kuona thamani ya fedha ambazo Serikali imewekeza katika ujenzi wa miundombinu hii ya SGR”

Wajumbe wamefanya ziara kwa kutumia treni ya uhandisi ya mkandarasi wa mradi wa SGR ambapo walipata fursa ya kutembelea jengo la stesheni ya SGR mkoani Morogoro na Dar es Salaam na mabehewa ya kisasa ya SGR katika stesheni ya Pugu. Pamoja na kuona maendeleo ya mradi kipande cha Dar es Salaam – Morogoro ambacho kimefika zaidi ya asilimi 97 walipata taarifa fupi ya Shirika pamoja na mradi kwa ujumla.

Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Dar es Salaam na Mjumbe wa Kamati Mhe. Janeth Masaburi amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwani amefanya kazi kubwa katika miaka miwili ya uongozi wake.

“Tumetembelea yale mabehewa ambayo watu walikuwa wanayabeza, ni mabehewa mapya, mazuri yenye viwango vya kimataifa, kikubwa tunachotakiwa kufanya ni kumpa nguvu Mhe. Rais“ aliongeza Mhe. Janeth

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa ameishukuru kamati ya PAC kutembelea mradi wa SGR kwasababu ni miongoni mwa kamati zinazofanya kazi kwa karibu na TRC, lengo ni kuhakikisha fedha zinazotengwa zintumiwa katika matumizi sahihi.