Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​KAMATI YA BUNGE YAITAKA TRC KUWASIMAMIA WAKANDARASI WAWEZE KUMALIZA MIRADI KWA WAKATI


news title here
14
March
2023

Kamati ya Bunge ya Miundombinu yalitaka Shirika la Reli Tanzania - TRC kuhakikisha wakandarasi wanakamilisha miradi kulingana na muda uliopangwa kimkataba, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Selemani Kakoso ametoa kauli hiyo alipokuwa katika ziara kukagua mradi wa reli ya kisasa - SGR kutoka Dodoma hadi mkoani Morogoro, Machi 14, 2023.

Kamati ya Bunge ya Miundombinu imeanza ziara ya siku mbili kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kwa kutumia treni ya uhandisi ya mkandarasi kutoka Dodoma hadi Morogoro kwa lengo la kuona maendeleo ya mradi wa SGR ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya bunge la bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/2024.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Kakoso ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwaajili ya ujenzi wa mradi wa SGR ambao kukamilika kwake utaleta manufaa makubwa kwa watanzania. Kakoso ameahidi kuwa kamati itaendelea kuusemea vema mradi pamoja na kutetea bajeti ya utekelezaji wa mradi.

“Naishukuru Serikali kwa jitihada za kukamilisha mradi wa SGR, fedha nyingi zimewekwa pia yapo mambo ambayo tumeishauri Serikali ili mambo yaweze kwenda haraka, la kwanza ni Serikali kuhakikisha huu mradi unakamilika kwa wakati kulingana na mikataba bila kuchelewa kwani matumaini ya wananchi ni kuona mradi unaanza ili waweze kupata manufaa” alisema Mhe. Kakoso

Wajumbe wa Kamati ya Bunge walipata fursa ya kukagua jengo la ofisi ya makao makuu ya TRC linalojengwa eneo la Kikuyu Kusini jijini Dodoma likiwa kwenye hatua za mwisho za ukamilishwaji. Shirika la Reli ni miongoni mwa taasisi za Serikali zinazotarajiwa kuhamia makao makuu ya Nchi jijini Dodoma katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali.

Pamoja na kukagua jengo la ofisi ya TRC wajumbe walitembelea na kukagua jengo la stesheni ya SGR jijini Dodoma na kupata maelezo ya kina kutoka kwa wataalamu kabla ya kuendelea na ukaguzi kuelekea mkoani Morogoro ambapo wajumbe walitembelea handaki refu la SGR, Stesheni ya Kilosa na Morogoro.

Mambo mengine ambayo kamati ya Miundombinu imeishauri Serikali ni kuhakikisha ununuzi wa vitendea kazi ikiwemo Vichwa, Mabehewa na Mitambo katika vipnde vingine vya mradi wa SGR vinaanza kushuhulikiwa mapema pia kuendelea kuandaa vijana wa kitanzania watakaosimamia mradi wa SGR pindi utakapoanza kufanya kazi kupitia mafunzo wakati wa ujenzi.

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. Atupele Mwakibete ameeleza baadhi ya changamoto zilizopelekea mradi wa SGR Dar es Salaam – Morogoro kuchelewa kuwa ni pamoja na ugonjwa wa UVIKO19 ambao kwa kiasi kikubwa ulipelekea kuchelewa kwa vitendea kazi ambavyo ni Vichwa, Seti za Treni na Mabehewa. Pamoja na changamoto hizo Mhe. Atupele amesema kuwa Serikali inatarajia kuanza uendeshaji wa reli kisasa Dar es Salaam – Morogoro baada ya kupokea vichwa na mabehewa mwezi Aprili 2023..

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Bi. Amina Lumuli amesema “Tumepokea ugeni wa kamati ya Bunge ya Miundombinu ambayo imetembelea mradi kutoka Dodoma hadi Morogoro na tutaelekea hadi Dar es Salaam ambapo maagizo makubwa tuliyopewa ni kuhakikisha tunakamilisha miradi kwa wakati na viwango vinahitaji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, sisi kama menejimenti tumeyapokea na tutayafanyia kazi”