Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​KAMATI YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA YATEMBELEA KARAKANA NA CHUO CHA RELI TABORA


news title here
18
March
2023

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma ikiongozwa na Mwenyekiti Mhe. Jerry Silaa imefanya ziara katika karakana ya vichwa vya treni na mabehewa na Chuo cha Reli Tabora (TIRTEC), Machi 17, 2023.

Lengo la ziara ni kujionea uwekezaji mkubwa, kazi zinazofanywa na Shirika la Reli Tanzania - TRC na kuangalia namna kazi zinazofanywa zinakwenda sambamba na ujenzi wa reli ya kisasa – SGR ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uendeshaji wa mradi.

“Tumetembelewa na kamati ya bunge ya uwekezaji wa mitaji ya umma, wametembelea karakana inayohusika na ukarabati wa vichwa vya treni na mabehewa, wameweza kutoka Stesheni kwenda Karakana kwa kutumia mabehewa mapya ya reli ya zamani - MGR ambayo yamekuja hivi karibuni lakini pia wametembelea Chuo cha Reli Tabora” alisema Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Bi. Amina Lumuli.

Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Jerry Silaa ameipongeza TRC kwa utendaji mzuri wa kazi, kwa kusimamia ujenzi wa vipande zaidi ya sita vya SGR, pamoja na karakana ya Tabora ambayo imejengwa muda mrefu na inaendelea kufanya kazi. Kamati imeweka msisitizo katika maeneo hayo kwasababu kwenye MGR kazi zinaendelea kufanyika na SGR ujenzi unaendelea kwa maslahi ya watanzania.

Mhe. Jerry amesema kuwa anaamini msingi wa chuo cha Reli Tabora ndio sura ya chuo kipya kitakachojengwa kuandaa watalaamu wa kusimamia SGR, pia kupitia uwekezaji wa SGR ambayo Serikali ya Rais Dkt. Samia imewekeza zaidi ya Shilingi Trilioni 23 za kitanzania unakwenda kuleta tija kupitia faida ya moja kwa moja vilevile faida mtambuka za maeneo mengine ya uchumi, kilimo na utalii.

“Kikubwa ni kwamba yale ambayo tumeyaelekeza kwa Shirika yanafanyiwa kazi, pia mashirika haya ya kimkakati tunakutana nayo mara kwa mara. Mwisho tunawapa pongezi, pale karakana tumeona vijana wanafanya kazi kubwa sana, lakini maelekezo ya chuo hiki kwa mkuu wa chuo na walimu wake kuendelea kuboresha mazingira haya yafanyiwe kazi” alisema Mhe. Silaa

Bi. Amina Lumuli amesema kuwa wajumbe wa kamati wameona kazi zinazofanyika, wameona wafanyakazi jinsi wanavyofanya kazi, wameona mifumo ya ufundishaji na mitaala ya chuo cha reli pia wametoa maelekezo kwa bodi, menejimenti na wafanyakazi kuhakikisha kwamba Shirika linakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ili kuwadhihirishia wananchi kuwa uwekezaji uliofanywa na Serikali unakwenda kuchangia kukuza uchumi na pato la taifa.