Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​KAMATI YA BUNGE YA PIC YARIDHISHWA KUANZA SAFARI ZA SGR


news title here
27
March
2024

Shirika la Reli Tanzania - TRC limepokea ugeni kutoka kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma - PIC na kufanya ziara ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro Machi 27, 2024.

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Mhe. Augustine Vuma alisema kwa niaba ya kamati kuwa wameridhishwa na viwango vizuri vya miundombinu ya ujenzi huo.

“Mradi umejengwa katika viwango vizuri na vinavyostahili na safari zitakapoanza zitapunguza abiria kukaa kwa muda mrefu wakiwa safarini” alisema Mhe. Vuma.

Aidha, Mhe. Vuma alisema utekelezaji wa mradi umetoa ajira ya moja kwa moja zaidi ya elfu 30 na ajira ambazo sio za moja kwa moja 150,000 na kuwezesha kipato cha zaidi ya bilioni 650.

“Gharama za usafirishaji wa mizigo zitapungua kwa asilimia 40, kwa jinsi tulivyoshuhudia maelekezo ya Mhe. Rais ya kwamba treni ianze uendeshaji Julai mwaka huu inaenda kukamilika” alieleza Mhe. Vuma

Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya TRC Prof. Ally Karavina ameeleza kuwa majaribio yanaendelea vizuri na asilimia kubwa ya mradi kwa kipande cha kwanza umekamilika.

“Tuwaondoe hofu watanzania kwamba mradi huu wa kimkakati utaleta tija ya kukuza maendeleo ya taifa letu” alisema Karavina.

Naye Mkurugenzi Mkuu kutoka TRC Ndugu Masanja Kadogosa ameishukuru Kamati ya PIC kwa kuridhika baada ya kukagua mradi kwa kutumia treni ya umeme ya SGR pamoja na kuona mifumo ya uendeshaji inavyofanya kazi kwa uhakika.

“Kitu kikubwa ni sisi kuendelea kuchapa kazi ili kuhakikisha kwamba mwezi Julai safari za kutoka Dar Es Salaam hadi Dodoma zinaanza” alisema Ndugu Kadogosa.

Mradi wa SGR utaleta mageuzi makubwa kiuchumi katika taifa pamoja na nchi jirani kwa kusafirisha abiria na mizigo.