KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YATEMBELEA UJENZI WA SGR MWANZA – ISAKA, WAMPONGEZA RAIS SAMIA

March
2022
Kamati ya bunge ya kudumu ya miundombinu imetembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kipande cha tano cha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR Mwanza – Isaka, chenye jumla ya km 341, jijini mwanza. Machi 14, 2022.
Katika ziara hiyo sehemu ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya ujenzi nchini, kamati imetembelea kambi ya mkandarasi iliyopo eneo la Seke wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Kambi ya Fela wilayani Misungwi, Mwanza na kambi ya Malampaka ya Maswa mkoani Simiyu.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi mbele ya kamati hiyo meneja mradi wa ujenzi wa SGR Mwanza – Isaka, Mhandisi Machibya Masanja ameeleza kuwa mpaka sasa ujenzi katika kipande hicho umefikia 4.46%.
Aidha, akifafanua juu ya utofauti wa wakandarasi katika vipande tofauti vya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli ya kisasa, Mhandisi Machibya amesema kuwa utofauti huo hauwezi kupelekea utofauti wa viwango kwakuwa wakandarasi wote wanajenga kulingana na viwango vilivyoainishwa katika matakwa ya muajiri.
“tulilizingatia hilo kwasababu, kama tungekuwa na viwango tofauti katika vipande hivi vya mradi, wakati wa kuanza uendeshaji isingewezekana kupitisha treni moja kuanzia Dar es salaam hadi Mwanza, tunachokitaka hata kama reli itajengwa na wakandarasi watatu au wane tofauti, ionekane ni reli moja” alieleza Mhandisi Machibya.
Akieleza juu ya namna ambavyo majaribio ya ubora wa vifaa vya ujenzi yanavyofanyika katika mradi, Mkurugenzi wa Miundombinu ujenzi, Mhandisi Faustine Kataraia ameeleza kuwa zoezi hilo linafanyika kupitia maabara za mshauri Mwelekezi, maabara ya Chuo kikuu cha Dar es salaam na Shirika la Viwango nchini - TBS.
Kwa upande wake Naibu waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Atupele Mwakibete amesema kuwa hadi kufikia sasa uwekezaji wa serikali katika ujenzi wa Reli ya kisasa, umefikia Shilingi Trilioni 14.7 na kuwa wakandarasi wanalipwa kwa wakati.
“kuanzia kipande cha kwanza hadi hapa, hakuna mkandarasi anayedai na serikali imeshalipa zaidi ya Shilingi Trilioni 7” alisema Naibu Waziri Mwakibete.
Mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo katika kambi ya Mkandarasi ya Malampaka, Maswa mkoani Simiyu, mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Moshi Selemani Kakoso, amempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ambao mpaka sasa awamu ya kwanza inatekelezwa kwa vipande vinne vya ujenzi kati ya vitano.
Hata hivyo, Mhe. Kakoso amewataka wahandisi wazawa waliopewa dhamana ya kusimamia ujenzi wa reli ya kisasa, kuwa wazalendo ili kukamilisha mradi katika viwango vinavyohitajika.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRC, Prof. John Kondoro ameishukuru kamati kwa kutembelea na kukagua ujenzi wa kipande cha tano cha SGR Mwanza – Isaka na kueleza kuwa maelekezo na ushauri wa kamati hiyo ni chachu kwa TRC katika kuendelea kusimamia vyema ujenzi wa mradi huo wa kimkakati.
Utekelezaji wa kipande cha tano cha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa Mwanza – Isaka ulianza Mei 15, 2021 ambapo mpaka sasa maendeleo ya ujenzi yamefikia 4.46% huku faida mbalimbali zikitajwa kuambatana na utekelezaji wa mradi ikiwemo ajira na maendeleo ya sekta ya viwanda na uwekezaji.