KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YARIDHISHWA NA MAENDELEA YA MRADI WA SGR, WIZARA, TRC WAPONGEZWA
March
2023
Kamati ya Bunge ya kudumu ya Miundombinu yaridhishwa na maendeleao ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR baada ya kukamilisha ziara kukagua mradi kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam iliyofanyika kwa siku mbili kuanzia Machi 14 hadi 15, 2023.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso ameridhishwa na maendelea ya mradi kipande cha Morogoro – Makutupora ambacho kimefikia zaidi ya asilimia 82 na kipande cha Dar es Salaam - Morogoro ambacho kimefikia zaidi ya asilimia 97,kazi kubwa iliyobaki ni ujenzi wa reli kuelekea bandarini jijini Dar es Salaam.
“Nimeridhishwa na maendeleo ya mradi, naipongeza Wizara na TRC kwa kazi kubwa mliyofanya, nawaahidi mtakapoleta maombi yenu ili yaweze kuidhinishwa kupitia Wizara yako Mhe. Waziri sina shaka pamoja na Wabunge walioona kazi hii tutayapitisha bila kumkwamisha Mhe. Rais” alisema Mhe. Kakoso
Mhe. Kakoso alisisitiza kuwa “Tumefanya ukaguzi kutoka Dodoma hadi Morogoro na hatimaye tumefika Dar es Salaam, naipongeza Serikali kwa kazi ambayo imefanya kujenga miundombinu ya reli ya kisasa, dhamira ya Serikali tumeiona na tumejiridhisha”
Aidha, Kamati pia imefanya ziara katika Karakana ya Vichwa vya treni mkoani Morogoro kwa lengo la kukagua utendaji wa karakana hiyo pamoja na kuona namna ya kuishauri Serikali jinsi ya kuboresha ufanisi wa kazi katika karakana hiyo ili kuleta tija katika huduma ya usafirishaji kwa njia ya reli na kukuza uchumi.
“Tumekagua karakana ya reli inayokarabati na kutengeneza vichwa vya treni mkoani Morogoro, na leo tumekagua reli kwakweli miundombinu inajengwa niwahakikishie wananchi kuwa ujenzi umefikia hatua nzuri sana” alisema Kakoso
Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. Atupele Mwakibete ambaye aliambatana na Kamati katika ziara ameishukuru kamati na kusema kuwa kwa niaba ya ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ameyapokea maelekezo na ushauri ikiwemo suala la mabehewa na vichwa vya treni ambalo linaendelea kufanyiwa kazi ambapo hadi kufikia mwezi Aprili 2023 vichwa vya treni vinatarajiwa kuwasili ili kuanza kutoa huduma ya usafiri Dar es Salaam – Morogoro.
“Nichukue fursa hii kwa kuishukuru kamati ya bunge ya miundombinu kwa kulitembelea Shirika letu la reli lakini pia kwa maoni yao na mara kadhaa wamekuwa wakitoa maoni na Serikali imekuwa ikiyafanyia kazi, nawapongeza watumishi wote na Mwenyekiti wa Bodi pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TRC kwa usimamizi mzuri”
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Kondoro amesema kuwa amefarijika na maelezo na maelekezo ya kamati kwani inaashiria kuwa wameridhika na maendeleo ya mradi, pia maelekezo ambayo yametolewa na kamati Uongozi wa Shirika umeyapokea kwaajili ya kuyatekeleza
Kamati imetoa ushauri kwa Serikali ikiwemo kuongeza kasi ya ukamilishaji wa mradi, kuweka mazingira ya kuajiri wafanyakazi ambao watakwenda kuendesha mradi, kusimamia ununuzi wa vitendea kazi ikiwemo mitambo, mabehewa na vichwa vya treni pia kamati imeitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ishirikiane na Wizara ya Nishati ili kuwepo na nishati ya uhakika itakayowezesha shughuli za uendeshaji wa reli ya kisasa