KAMATI YA BUNGE YA BAJETI YAIPONGEZA WIZARA YA UCHUKUZI NA TRC
.jpg)
March
2022
Kamati ya Bunge ya Bajeti ikiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Daniel Sillo imefanya ziara kukagua mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kipande cha Dar es Salaam – Morogoro kuanzia stesheni ya Dar es Salaam hadi Soga mkoani Pwani Machi 7, 2022.
Lengo la ziara hiyo ni kufanya ukaguzi kwaajili ya kujiridhisha na matumizi ya fedha zinazotengwa kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa. Kamati imefanya ukaguzi huo ikiwa ni hatua mojawapo kuelekea maandalizi ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023.
“Lengo la ziara hii ni kutembelea miradi mingi ya kimkakati ambayo serikali imeweka fedha nyingi na hivi leo tumetembelea mradi huu wa SGR kuona fedha zilizotengwa kama zinafanya kazi iliyopangwa na tumeona kazi nzuri imefanyikakatika kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km300) imekamilika kwa 95.3%, tunaipongeza serikali ya CCM chini ya Rais Samia Suluhu Hassan lakini pia wizara na TRC tunawapongeza sana” alisema Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Daniel Sillo
Mhe. Sillo amesema kuwa ujenzi wa reli ya kis asa ni muhimu kiuchumi na kijamii, kwa kuwa ujenzi huu unaunganisha Bandarina nchi jirani na kuongeza kuwa kamati hiyo itaendelea kuishauri serikali kutoa fedha kwaajili ya kutekeleza mradi huu mkubwa kwaajili ya maendeleo ya Taifa na mtu mmoja mmoja.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Atupele Mwakibete ameishukuru kamati ya bunge ya bajeti kutembelea mradi wa SGR ambayo ilianza ukaguzi katika stesheni ya Dar es Salaam hadi Soga na imeridhika namna ambavyo serikali imewekeza na kueleza kuwa Serikali imeweka na inaendelea kuweka fedha nyingi katika mradi huo.
“Nimpongeze sana Mhe. Rais Samia kwa kuendelea kutafuta fedha na kuhakikisha mradi wa reli ya kisasa unakamilika, ni zaidi ya Trilioni 7 zimeshalipwa na hakuna mkandarasi anayedai lakini pia ni zaidi ya Trilioni 14.5 ambazo tumeingia mikataba mbalimbali katika vipande, kwa msingi huo naamini katika bunge lijalo litaidhinisha fedha ili watanzania wapate huduma bora” aliongeza Mwakibete
Naye Mkurugenzi wa Shirika la reli Tanzania Masanja Kadogosa ameshukuru ujio wa kamati hiyo kwakuwa Serikali iko katika mpango wa kuandaa bajeti ya mwaka 2022/2023 hiyo ujio wa kamati hiyo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuiaminisha kamati hiyo kuhusu kile kinachofanyika
“Tunaishukuru kamati yetu ya bajeti kuja kututembelea, sasa tuko kwenye harakati za kuandaa bajeti, kwahiyo inavyokuja na kujionea kazi inakuwa ni rahisi sana kuwaelezea kwa sababu wameshaona”, alisema Kadogosa
Akifafanua kuhusu fedha zinazotumika katika utekelezaji wa mradi wa SGR Kadogosa ameeleza kuwa “Ujenzi tulianza na pesa ya ndani lakini baadaye tulipata fedha kutoka taasisi za kifedha na ndio utaratibu tunaoendelea nao, hata kwa kipande tunachoanza nacho sasa Makutupora – Tabora hivi karibuni tayari tumeshalipa malipo ya awali Bilioni 600 ambazo zimetoka ni fedha za ndani, na Serikali inaendelea kutafuta fedha kuongeza nguvu”