Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

JAMII YA WAFUGAJI MOROGORO VIJIJINI YAPEWA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA VIVUKO KUEPUSHA UHARIBIFU WA MIUNDOMBINU YA SGR


news title here
14
August
2021

Shirika la Reli Tanzania - TRC likiendelea na kampeni ya uelewa kwa jamii kuhusu usalama na ulinzi wa miundombinu ya Reli ya kisasa – SGR limekutana na jamii ya wafugaji mkoani Morogoro vijijini kuendesha semina elekezi kuhusu matumizi sahihi ya vivuko vya mifugo ili kuepusha uharibifu wa miundombinu ya reli ya kisasa, hivi karibuni Agosti, 2021.

Maafisa kutoka kitengo cha ulinzi na usalama wa reli TRC walifika katika vijiji vya Kidugalo, Mgude na Sinyaulime na kufanya mazungumzo wa viongozi wa Serikali ya kijiji na mitaa na kubaini changamoto nyingi ambazo zinawakabili wananchi hao ikiwemo matumizi sahihi ya vivuko kwa ajili ya mifugo.

Aidha, jamii hiyo ya wafugaji imekuwa na desturi ya kutotumia vivuko vilivyowekwa na kuvusha mifugo juu ya tuta la reli hali inayopelekea uharibifu wa miundombinu ya reli ikiwemo kuharibika kwa tuta, kutawanyika kwa kokoto, nyasi zilizopandwa pembeni mwa tuta la reli kuliwa na mifugo na kusababisha mmomonyoko wa udongo katika tuta la reli.

Kutokana na changamoto hiyo, Maafisa wa ulinzi na usalama wa reli waliwataka viongozi hao kuandaa mkutano na wananchi wakiwemo wafugaji kwa ajili ya kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya vivuko ili kuepusha madhara makubwa yatokanayo na uharibifu na uhujumu wa miundombinu ya reli ya kisasa.

Mhandisi Fredirick Kitaly kutoka kitengo cha ulinzi na usalama wa reli aliwataka wananchi wote kwa ujumla wakiwemo na wafugaji kuacha kuvunja sheria na kufuata alama zilizowekwa ambazo zinaelekeza maeneo sahihi ya kuvusha mifugo na maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya watu kuvuka.

“Ndugu wananchi wale wenye mifugo kama nilivyoeleza madhara makubwa ambayo yatajitokeza msipofuata taratibu wa kuvuka na kuvusha mifugo. Ninawaomba muache kuvuka na kuvusha mifugo juu ya tuta la reli tumewajengea vivuko na tumeweka alama kama muongozo wa kuwaonesha wapi ni sehemu sahihi ya kuvukaa” alisema Mhandisi Kitaly.

Wananchi nao walipewa nafasi ya kueleza changamoto mbalimbali wanazopata wakati wa utekelezaji wa mradi wa SGR. Wananchi wengi hasa wafugaji walibainisha kuwa changamoto kubwa ni umbali pamoja na uchache wa vivuko hivyo kuwalazimu kuvuka na kuvusha mifugo juu ya reli.

Maafisa kutoka TRC waliwaomba wananchi kuanza kutumia vivuko hivyo na kuzingatia alama zinavyoelekeza “kipindi cha ujenzi wa vivuko hivyo Shirika liliwashirikisha viongozi wa ngazi za vijiji na kata katika kutoa maamuzi wapi vivuko viwekwe kutokana na uhitaji wa jamii nzima na idadi kubwa ya watumiaji kwa kuzingatia usalama wao” aliongeza Mhandisi Kitaly.

Hata hivyo Maafisa waliwasihi wananchi sambamba na wafugaji kuendelea kuwa wavumilivu kwa kufuata sheria kipindi ambacho changamoto hizo wanapozipeleka kwa viongozi wa Shirika la reli ili waweze kutatua na kutoa suluhisho la changamoto hizo walizozisema ili jamii ibaki salama na kunufaika na mradi wa SGR.