HUNDI 799 KULIPWA KWA WANANCHI KUPISHA UJENZI WA SGR MWANZA- ISAKA

November
2021
Shirika la Reli Tanzania - TRC limeanza zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi ili kuanza ujenzi wa njia kuu ya reli ya kisasa kipande cha tano Mwanza - Isaka lililofanyika katika maeneo ya Nyashimba , Sekebugolo na Muhida mkoa wa Shinyanga na Simiyu hivi karibuni Novemba , 2021.
Mthamini kutoka TRC Bw. Valentine Baraza amesema kuwa ujenzi huo wa njia kuu ya SGR kipande cha Mwanza - Isaka unatarajiwa kuanza mara baada ya wananchi ambao tayari wameshalipwa stahiki zao kuhama kulingana na makubaliano ya mkataba anaepatiwa mwananchi wakati akipokea hundi.
“Mkataba unamtaka mwananchi kuhama katika eneo ndani ya siku zisizozidi kumi na nne” alisema Bw. Baraza.
Pia Bw. Baraza alisisitiza kuwa wananchi kufuata taratibu na kutumia muda uliopangwa kuhamisha makazi yao ili kuepusha usumbufu baina yao na mkandarasi pindi anapotaka kuanza ujenzi.
“Maeneo ambayo yamechukuliwa ni pamoja na majengo, mazao, viwanja pamoja na mashamba” alieleza Bw. Baraza.
Pia Afisa Ardhi kutoka wilaya ya Maswa Bi. Grace Mgombera amesema kuwa zoezi la kuomba ardhi kwa wananchi limeenda vizuri bila mgomo wowote na pia wamepokea mradi huo wa SGR katika maeneo yao ili kuweza kukuza maendeleo ya wananchi na nchi.
“Kiukweli wananchi wamefurahi sana kusikia reli ya kisasa itapita katika maeneo yao na wametoa ushirikiano mkubwa” alisema Bi. Grace.
Naye mwananchi kutoka Muhida wilayani Simiyu Bw. Samwel Bugado amefurahishwa na serikali kulipa fidia hizo kwa wakati na kusema kuwa kiasi cha fedha alichopata kitamsaidia kusomesha watoto wake katika elimu ya juu na kufanya maendeleo ya biashara.
Zoezi hilo la ulipaji wa fidia ni endelevu ambalo litafanyika katika maeneo mbalimbali kwa takribani kilometa 46 kwa kipande cha tano Mwanza - Isaka.