Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​HEKO TRC KUSIMAMIA VYEMA MRADI WA KIMKAKATI WA SGR; WANANCHI MWANZA


news title here
30
December
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la utwaaji ardhi kupisha ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha tano Isaka - Mwanza linalofanyika mtaa wa Mkuyuni Sokoni wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza Disemba, 2022.

Wananchi katika mtaa wa Mkuyuni Sokoni wametoa pongezi kwa Shirika la Reli Tanzania kwa kuendelea kusimamia vyema mradi huo wa kimkakati wa SGR na kufuata taratibu zote zinazostahili, kufuatia zoezi la uhamishaji makaburi linalofanyika katika mtaa huo.

Msimamizi wa SGR kipande cha tano Isaka - Mwanza Mhandisi Blasius Mwita ameeleza kuwa TRC inafuata taratibu zote zilizopo katika ukamilishaji wa zoezi hilo kupitia wataalamu kutoka wizara ya afya katika eneo husika.

“Wataalamu wa afya kutoka halmashauri ya wilaya ya Nyamagana ndio wenye jukumu la kuhamisha makaburi, sisi TRC tunasimamia na kuwezesha ili zoezi liende kwa ufasaha” alisema Mhandisi Mwita.

Mhandisi Mwita alisema kuwa TRC inasimamia zoezi hilo kuhakikisha mahitaji yote yanayohitajika yanapatikana kwa wakati ikiwemo vifaa kama majembe, surulu, koleo, madawa, pampu, sanda, mifuko, majeneza na mashahidi, gloves, maski, ovaroli na mabuti.

“Tunahakikisha tunatoa malipo kwa kila aliyeshiriki kufanya kazi katika zoezi kuanzia vibarua, wananchi, mbao, maafisa afya, viongozi wa dini, mwenyekiti na mtendaji wa mtaa husika, madereva na viongozi wengine“ alisema Mhandisi Mwita.

Mhandisi Mwita aliongezea kuwa ”makaburi hayalipwi fidia ila tunatoa kifuta machozi chenye thamani ya laki tatu, isipokua kaburi lililojengewa linafanyiwa uthamini tofauti”.

Afisa afya kutoka Halimashauri ya jiji la Mwanza Bi. Sophia Kiluvya alisema kuwa jukumu lao kubwa ni kuhakikisha taratibu zote za kiafya zinazingatiwa ili kuepusha madhara ya kiafya kwa watu.

“Tunamwaga dawa maalumu katika eneo lote ili kuua vijidudu visisambae na kuleta madhara” alisema Bi. Sophia.

Bi. Sophia alieleza kuwa vibarua wote wanapatiwa vifaa kinga zikiwemo ovaroli, gambuti, kikinga mikono (gloves) ili kujikinga wakati wanaendelea na zoezi.

“Vibarua hua wanavua maski kwasababu ya kukosa hewa safi (Oxygen) hasa kwa kazi yao ambayo wanatumia pumzi nyingi hivyo tunamwaga madawa kwanza kuua vijidudu visizambae hewani” alieleza Bi. Sophia.

Pia mwananchi kutoka katika mtaa wa Mkuyuni Sokoni Bw. Halfan Salim alisema kuwa mradi huo utaleta manufaa kitaifa na kuipongeza TRC kusimamia vyema zoezi hilo na kuwa na usalama baina ya ndugu na viongozi wa serikali ya mtaa na kusimamia taratibu zote za kupumzisha wapendwa wao.

Zoezi hilo ni endelevu mpaka makaburi yote yaliyopitiwa na mradi huo kuhakikisha yameondolewa katika eneo hilo la Mkuyuni Sokoni jijini Mwanza.