Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

FIDIA TRC CHACHU YA MAENDELEO


news title here
09
January
2024

Shirika la Reli Tanzania limeendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi ambao ardhi zao zimetwaliwa kupisha ujenzi wa miundombinu ya Reli ya Kimataifa ya SGR katika kipande cha tatu Makutupora -Tabora hivi karibuni ,Januari, 2024.

Katika zoezi hilo la ulipaji fidia takribani wananchi 70 kutoka katika vijiji vya Azimio, Nyahua, Kimungi, Kazaroho, Genge 8 , Kawekapina , Ntulu, Lekatugeme , Aghondi na Tabora Mjini wamelipwa fidia zao ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya njia kuu ya Reli ( Right of way) ya SGR katika kipande cha tatu cha Makutupora -Tabora.

Akiongea wakati wa zoezi la ulipaji fidia mratibu wa kazi za utwaaji ardhi na fidia kipande cha tatu BW . Mjandwa Misango kutoka TRC amesema kuwa katika kuhakikisha kila mwananchi ambae ardhi yake imetwaliwa analipwa stahiki zake kwa haki zoezi la ulipaji fidia linafuata taratibu mbalimbali za kisheria na kanununi za utwaaji ardhi.

Taratibu hizo ni pamoja na ukaguzi wa awali ambapo njia ya Reli itapita, kubainisha na kukagua Mali za wananchi , ukokotoaji fidia na mwisho zoezi la ulipaji fidia .

"kabla zoezi la ulipaji fidia halijafanyika ,timu ya wataalamu kutoka sekta mbalimbali zinahakikisha ukaguzi na vielelezo vyote vinakuwa sawa kisheria ili kuhakikisha wananchi wanapata haki na kuondoa migogoro katika jamii" Alisema Bwana Misango.

Nae Bwana Francis Masaka kutoka katika kijiji cha Aghondi wilaya ya Itigi amesema kuwa wananchi wa Aghondi wanaunga mkono Serikali kwa ujenzi wa Reli ya SGR kwani itaenda kukuza sekta ya kilimo ,biashara na ukuaji wa mji wa Itigi kwa ujumla.

"Itigi Sisi ni wakulima wa mahindi na Alezeti ,Serikali imefanya Jambo muhimu Sana kujenga SGR, hii Reli ikikamilika Itigi itakua kubwa sana ,viwanda vya mafuta vitajengwa ,soko la mafuta ya Alezeti litaongezeka ,Sisi tunaunga mkono na tunaomba ikamilike mapema"Alisema Bwana Masaka.