Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​FIDIA ZA MRADI WA SGR ZAWANUFAISHA WANANCHI KANDA YA ZIWA


news title here
29
August
2023

Fidia zinazolipwa na Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania – TRC kwa wananchi waliotwaliwa maeneo yao kupisha mradi wa ujenzi wa reli yenye kiwango cha kimataifa – SGR kipande cha Mwanza - Isakaz aleta faida na kuboresha maisha ya wananchi wa mikoa ya Shinyanga, Mwanza na Simiyu, Agosti 2023.

Wananchi wamebainisha suala hilo kupitia zoezi la malipo ya fidia linaloendelea katika vijiji zaidi ya 50 ya mikoa ya Mwanza, Simiyu na Shinyanga ambapo zaidi ya Shilingi Bilioni moja zinaendelea kulipwa kwa wananchi waliotwaliwa maeneo na mali zao kupisha mradi wa SGR.

Faida zilizobainishwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba bora za kisasa, kukuza na kuendeleza shughuli za kilimo, ufugaji na biashara ambazo zinategemewa kwa kiasi kikubwa na wakazi wa maeneo husika.

“Kupitia fidia wananchi wameweza kujenga nyumba za kisasa na kupelekea kuboresha maisha yao, vilevile uzalishaji kupitia shughuli za kilimo umeongezeka kwani wapo baadhi ya wananchi wamenunua mashamba, vifaa, na pembejeo za kilimo pia kwa upande wa biashara wananchi wameweza kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza mitaji yao” alisema Bwana Zakayo Pastory, mkazi wa kijiji cha Ligembe

Pamoja na faida kadhaa zilizoonekana kupitia zoezi la ulipaji wa fidia tangu kuanza kwa mradi, Viongozi na Wananchi wamekuwa mstari wa mbele kutoa ushirikiano kutokana na kutambua umuhimu na faida za mradi pamoja na fidia zinazolipwa na Serikali ili ktekeleza mradi.

“Faida ni nyingi, hizi tunazoziona hivi sasa ni sehemu tu ya faida kwa tumeona miji na vijiji vikikua kwa kasi kutokana na utekelezaji wa mradi huu, kwa upande wetu sisi ambao maeneo yatu yametwaliwa tunaiponeza Serikali kwa sababu tumeanza kula matunda ya mradi. Ushahidi upo wa kutosha ni namna

gani fidia hizi zinatunufaisha kwa kujenga nyumba za kisasa na kuendeleza shughuli za kiuchumi” alisema mtendaji wa kijiji cha Liboja, Bwana Takesh Simon

Mradi wa SGR umetoa faida nyingi wakati wa ujenzi ikiwemo ongezeko la ajira kwa wazawa katika sekta na fani mbalimbali, uboreshaji wa huduma za kijamii ikihusisha ujenzi wa shule, vituo vya afya na ujenzi wa barabara katika maeneo yanayopitiwa na mradi. Baada ya mradi kukamilika itasaidi uokoaji wa muda kwa usafiri wa abiria na mizigo na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mradi wa SGR Mwanza – Isaka unaendelea vema chini ya Mandarasi kampuni ya CCECC ya China ambapo umefikia 38.83% hadi mwezi Julai 2023. Kazi zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa tuta, vituo vya abiria, ujenzi wa madaraja na makalavati pamoja na uwekaji wa mataruma, reli na nguzo za umeme katika baadhi ya maeneo.

Shirika la Reli Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi limekuwa likiendesha mazoezi ya utwaaji ardhi tangu kuanza kwa mradi wa ujenzi wa SGR jijini Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu na Mwanza ili kuwezesha upatikanaji wa maeneo ya ujenzi wa mradi bila kuathiri Maisha ya wananchi. Hatua za awali za zoezi la fidia ni pamoja na uthamini ambao hufanyika wazi kwa kutambua mali na maeneo yanayotwaliwa pamoja na kuwashirikisha wahusika wakati wa uthamini.